RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema Serikali yake imejipanga kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola na hivyo kuwataka Watanzania wasiwe ma hofu na kuendelea kufanya shughuli zao. Rais Kikwete aliyasema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akiwahutubia wazee wa mkoa huo ikiwa ni utaratibu wake wa kulihutubia taifa kila mwezi.
“…Tumejipanga vizuri kuzuia ugonjwa huu (Ebola) usiingie Tanzania. Tumechukua tahadhari na kujiandaa vilivyo kukabiliana na janga hili kwa kuchukua hatua zifuatazo: Tunacho Kikosi Kazi cha Taifa kinachoongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donald Mbando cha kukabiliana na ugonjwa huu katika ngazi ya taifa hadi Wilaya, tumekamilisha mpango wa kitaifa “Ebola Contingency Plan” na tumetenga Shilingi milioni 500 ikiwa ni fedha za awali za utekelezaji wa mkakati huo.”
Akifafanua zaidi Rais Kikwete alisema Serikali imeandaa vifaa “personal protective equipment” kwa watumishi wa afya katika mikoa yote, wilaya zote, hospitali zote za Rufaa na kanda 37, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar. Tumesambaza pia dawa. Tumetenga kituo maalum tengefu (isolation unit) cha Wilaya ya Temeke na vituo vingine tengefu mikoani.
Aidha aliongeza kuwa mitambo maalum ya vipima joto na dalili za wagonjwa wa Ebola katika viwanja vya Mwalimju Nyerere (2), Mwanza (1), Zanzibar (1) na kituo cha Namanga (1) imewekwa na pia kuagizwa scanners 5 ambazo zimekwishawasili na zitafungwa katika viwanja vya ndege kwa ajili ya kujihami zaidi na ugonjwa huo.
“…Tangu mwezi Aprili, 2014 nchi za Afrika Magharibi hususan nchi ya Guinea, Siera Leone, Liberia na Nigeria zimekumbwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa hatari wa Ebola. Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa tayari watu 3,500 wameambukizwa na tayari zaidi ya vifo 1,900 vimetokea. Asilimia 40 ya vifo hivi vimetokea ndani ya wiki tatu hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2014. Ebola ndiyo virusi hatari zaidi duniani kuliko hata UKIMWI.”
Aidha alisema wataalam wa ugonjwa huo wanasema virusi vya Ebola hubebwa na ndege aina ya popo na wanadamu huupata kupitia kwa wanyama walioambukizwa kwa kuwagusa au kuwala. Anawataja wanyama hao ni pamoja na sokwe, nyani na swala. Maambukizi kutoka kwa mgonjwa huenda kwa mtu mwingine kwa kugusa damu au majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo au kwa kugusa maiti ya mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa huo.
“…Ugonjwa huu ni hatari sana kiasi kwamba hata watoa huduma za afya kama madaktari na wauguzi kama hawakuchukua tahadhari zinazotakiwa wanaweza kuambukizwa na hata kufa. Mpaka hivi sasa Daktari mmoja aliyekuwa anawahudumia wagonjwa wa Ebola kule Liberia amekufa. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mgonjwa kuwa na homa kali ya ghafla, kulegea mwili, kuumwa na kichwa, kuumwa na misuli na kutokwa na vidonda kooni.”
“…Dalili hizi zinaweza kuambatana na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele, kutokwa na damu ndani na nje ya mwili na kushindwa kufanya kazi kwa figo na ini. Dalili za ugonjwa huu hujitokeza katika siku 2 hadi 21 baada ya kuambukizwa. Tunamshukuru Mungu kwani mpaka sasa hapa nchini hajapatikana mtu yeyote mwenye ugonjwa huu.”
Raisa Kikwete alisema kati ya wagonjwa wanne waliohisiwa kuwa na Ebola ambao uchunguzi ulionesha hawakuwa na ugonjwa huo. Watatu kati ya wagonwja hao walikuwa ni wagonjwa wa malaria na mmoja uchunguzi wake bado unaendelea. Alisema wagonjwa wawili ni kutoka Dar es Salaam na wawili ni kutoka Geita na Nkasi.
Aliongeza kuwa wagonjwa hao waliohisiwa walihudumiwa na walifanyiwa uchunguzi kwa kufuata tahadhari zote za ugonjwa wa Ebola. Hii imeonesha utayari wetu wa kukabiliana na janga hili. Pamoja na kutokuwepo kwa mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitika kuwa na ugonjwa huu. Tumejipanga vizuri kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini.
“…Tunacho Kikosi Kazi cha Taifa kinachoongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Donald Mbando cha kukabiliana na ugonjwa huu katika ngazi ya taifa hadi Wilaya. Tumekamilisha mpango wa kitaifa “Ebola Contingency Plan” na tumetenga Shilingi milioni 500 ikiwa ni fedha za awali za utekelezaji wa mkakati huo. Tumeshaagiza Timu za Maafa za mikoa na wilaya kutekeleza mpango huo. Tumesambaza vifaa “personal protective equipment” kwa watumishi wa afya katika mikoa yote, wilaya zote, hospitali zote za Rufaa na kanda 37, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Zanzibar. Tumesambaza pia dawa.
“…Tumetenga kituo maalum tengefu (isolation unit) cha Wilaya ya Temeke na vituo vingine tengefu mikoani. Tumechukua tahadhari kubwa kwenye viwanja vya ndege. Tumekwishafunga mitambo maalum ya vipima joto na dalili za wagonjwa wa Ebola katika viwanja vya Mwalimju Nyerere (2), Mwanza (1), Zanzibar (1) na kituo cha Namanga (1). Tumeagiza pia scanners 5 ambazo zimekwishawasili na zitafungwa katika viwanja vyetu. Tumetoa mafunzo kwa watumishi wa afya wa mipakani na viwanja vya ndege. Tumetoa mafunzo hayo kwa watumishi 100 wa Dar es Salaam na 45 kutoka mikoa ya Arusha, Kagera, Rukwa, Mwanza, Kilimanjaro, Kigoma na Zanzibar. Tumepeleka watumishi watatu nchini Jamhuri ya Kongo kupata mafunzo maalum.” Alisema Kikwete.
Akizungumzia uboreshaji elimu Rais Kikwete alisema kuwa maandalizi ya kuboresha maabara ili kufanya uchunguzi wa sampuli nchini yamefanywa na kuongeza kuwa kwa sasa, eneo zima la Afrika Mashariki linategemea na kutumia maabara ya Nairobi.
Aliongeza kuwa viongozi wa ngazi zote hizi wamepatiwa mwongozo wa utekelezaji. Tunachoomba ni ushirikiano wa wananchi wote katika kuchukua tahadhari na kutoa taarifa mapema iwezekanavyo mara tu mnapogundua dalili za ugonjwa huu kwa mtu ye yote.
Mchakato wa Katiba
Nilipozungumza na Taifa mwishoni mwa mwezi Julai, nilizungumzia mchakato wa Katiba. Nilielezea utayari wangu wa kufanya kila liwezekanalo kusaidia kufanikisha mchakato wa Katiba unaonndelea sasa. Kwa moyo huo, sikusita, nilipoombwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (Umoja wa Vyama vyenye Uwakilishi Bungeni) Mhe. John Momose Cheyo kukutana nao na kufanya mazungumzo ya mashauriano.
“..Kama mnavyojua tulikutana tarehe 31 Agosti, 2014 Mjini Dodoma. Tumekuwa na mazungumzo mazuri. Tumepeana kazi ya kufanya na tumekubaliana kukutana tena tarehe 08 Septemba, 2014 kuendelea na mazungumzo yetu. Kinachotia moyo ni ule ukweli kwamba kila upande umeonesha kiu na utayari wa kuzungumza. Tuyape nafasi mazungumzo haya yatutoe hapa tulipo na kutusogeza mbele kwa umoja na mshikamano,” alisema Kikwete.