AKIWA nchini Australia Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Australia, Bwana Tony Abbot ambaye alimpongeza kwa kuamua kukabidhi madaraka kwa kiongozi mwingine kwa mujibu wa Katiba nchini Tanzania.
Rais Kikwete pia alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Gavana Mkuu wa Australia Mheshimiwa Peter Cosgrove, kabla ya kukutana na wawekezaji wakubwa wa Australia ambao tayari wanawekeza nchini Tanzania ambapo walizungumzia namna ya kuendeleza sekta mpya ya gesi nchini na jinsi Tanzania inavyoweza kunufaika kutokana na kupata gesi. Tayari Serikali ya Australia na makampuni binafsi ya gesi na mafuta, yanaisaidia Tanzania hasa katika vyuo vya ufundi stadi VETA na tafiti mbalimbali katika Kilimo.
Rais Kikwete alihitimisha ziara yake kwa kutunukiwa digrii ya udaktari wa heshima ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle, kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika uongozi kwa kipindi cha miaka 10 aliyokaa madarakani nchini Tanzania na Dunia kwa ujumla.