Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete jioni ya leo, Januari 9, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Rais wa Gambia, Yahya A. Jammeh.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, mjumbe huyo maalum, Lamin Kaba ambaye ni Waziri wa Uvuvi, Maliasili na Masuala ya Bunge amemkabidhi Rais Kikwete ujumbe maalum kutoka kwa Rais Jammeh.
Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete na Kaba wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Gambia na pia masuala ya Afrika na ya kimataifa. Mjumbe huyo maalum anatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Nairobi, Kenya ambako anatarajiwa kukutana na viongozi wa nchi hiyo.