Rais Kikwete Apokea Kombe la Dunia – Tanzania

Rais Jakaya Kikwete akinyanyua kombe la dunia.

Rais Jakaya Kikwete akinyanyua kombe la dunia.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ujio wa Kombe la Soka la Dunia katika Tanzania ni deni kubwa ambalo Watanzania wanatakiwa kulilipa kwa kuzinduka na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa mpira wa Tanzania hautaweza kuendelea hadi viongozi wa soka watakapoacha mchezo wa kuwekeza katika migogoro na kujiendeleza binafsi badala ya kuwekeza katika kuendeleza vipaji. Rais Kikwete pia amesema kuwa watanzania wameingiwa na ugonjwa wa kuona kila kitu ni changamoto ambazo wanatengeneza wao wenyewe na hatimaye kushindwa kuzimaliza.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza hayo Novemba 29, 2013, kwenye Uwanja wa Michezo wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya kupokea Kombe la Soka la Dunia ambalo liko kwenye ziara ya nchi sita za Afrika. Kombe hilo ni mali ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Rais Kikwete aliwaambia mamia ya wapenzi wa soka waliohudhuria hafla hiyo kwenye uwanja huo kuwa inashangaza kuwa FIFA linaendelea kuipa Tanzania upendeleo wa kupokea Kombe la Dunia wakati Tanzania yenyewe iko chini sana katika soka la kimataifa.

“Hata unashindwa kujua hasa wakubwa hawa wanaona nini katika Tanzania. Nchi yetu yenyewe iko hoi katika michezo ya kimataifa. Wanaacha nchi zenye viwango vya juu na kuichagua Tanzania. Wanachotuambia ni kwamba na sisi tufanye jitihada za kuboresha kiwango chetu na tuonekane pia katika viwanja vya Kombe la Dunia.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Ujumbe mkubwa wa ujio wa Kombe hili ni kwamba sisi tuna deni – viongozi wa soka, wachezaji na washabiki – kuwa tuzinduke na kuanza kushinda ili huko mbele hata rais wetu wa miaka ijayo aweze kulipokea Kombe hili siyo kwa kupigwa picha kama mimi, isipokuwa kwa Tanzania kuwa Bingwa wa Dunia.”

Kuhusu uwekezaji katika kuinua kiwango cha soka, Rais Kikwete alisema: “Nimelisema hili mara nyingi na kila nikisema nyie mnakasirika lakini nitaendelea kulisema kuwa tuache kuwekeza katika migogoro na kujiendeleza binafsi. Badala yake tuwekeze katika kuinua viwango na vipaji.”

Rais amesema kuwa ili kuhalalisha kushindwa, Watanzania wamebuni neno zuri la changamoto. “Kila kitu kuna changamoto. Changamoto zenyewe wanazitegeneza wenyewe na wanashindwa kuzimaliza.”

Kombe la Dunia lilisimama Tanzania kwa siku mbili, likiwa katika ziara ya Bara la Afrika ambako linapitia katika nchi sita tu miongoni mwa nchi zote za Afrika. Nchi hizo ni Morocco, Algeria, Ghana, Kenya, Tanzania na Kenya. Baada ya Tanzania, Kombe hilo linapelekwa Afrika Kusini ambayo ni nchi ya mwisho ya Afrika kabla ya kupelekwa Brazil kwa ajili ya Sherehe za Kupangwa kwa Ratiba ya Fainali za Kombe la Dunia zinazofanyika mwezi ujao.

Baada ya hapo, Kombe hilo linalopitishwa katika nchi 88 duniani litapelekwa Mashariki ya Kati. Hii ilikuwa mara ya tatu mfululizo kwa Kombe hili ambalo limetengenezwa kwa dhahabu tupu kupitishwa Tanzania na kupokelewa na Rais Kikwete.

Rais alipokea kombe hilo mwaka 2006 na Novemba 19, mwaka 2009 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Rais Kikwete alilishukuru Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Kampuni ya Coca Cola kwa kulileta tena Tanzania Kombe hilo. Tokea mwaka 1978, Kampuni ya Coca Cola imekuwa mdhamini rasmi wa FIFA katika kundi la viwanja visivyo na kilevi.