Rais Kikwete Apokea Hati za Utambulisho za Mabalozi Wanne

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati za utambulisho toka kwa balozi wa Slovak, Michal Mlynar April 25, Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akimsindikiza Balozi wa Ugiriki nchini, Elefthereios Kouvaritakis baada ya kupokea hati zake za utambulisho na kisha kufanya naye mazungumzo April 25, Ikulu jijini Dar es Salaam

Rais Dk Jakaya Mrisho Kikwete akitambulishwa na Mkuu wa Itifaki Balozi Mohamed Maharage kwa Balozi wa Kuwaite nchini Yacoub Y. Alsanad kabla ya ya kupokea hati zake za utambulisho na kisha kufanya naye mazungumzo Aprili 25, Ikulu jijini Dar es salaam.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Aprili 24, 2013, amepokea hati za utambulisho za mabalozi wanne ambao wataziwakilisha nchi zao katika Tanzania kwenye shughuli iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Mabalozi hao ambao wote wana makazi yao Nairobi, Kenya ni Balozi Abdelilah Benryane wa Morocco, Balozi Sandor Juhazs wa Hungary, Balozi Christian Hasenbichler wa Austria na Balozi Konrad Paulsen wa Chile.

Katika mazungumzo yake na Balozi Benryane, Rais Kikwete amemwomba Balozi huyo amkumbushe Mfalme Mohammed VI kuwa mwaliko wake wa kuitembelea Tanzania wakati na muda wake utakaporuhusu bado upo pale pale na kuwa Tanzania inasubiri kwa hamu kumpokea Mfalme.

Naye Balozi Sandor Juhazs amemwambia Rais Kikwete kuwa Hungary imedhamiria kikwelikweli kurudisha uhusiano wake wa zamani wa karibu wa utamaduni na elimu na Tanzania kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Dhamira ya nchi yangu katika muongo mmoja unusu uliopita imekuwa ni kuongeza nguvu ya kuimarisha upya uhusiano wetu na Afrika na kwa upande wa Tanzania tungependa kurudisha ukaribu wetu katika elimu na utamaduni,” Balozi Juhazs amemwambia Rais Kikwete.

Katika mazungumzo na Balozi Hasenbichler, Rais Kikwete ameipongeza Austria kwa jinsi inavyotimiza majukumu yake ya kimataifa kupitia mashirika mbali mbali ya kimataifa yenye makazi yake nchini humo likiwamo Shirika la Kimataifa la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) lenye makao yake makuu mjini Vienna, nchini humo.
“Austria ni nchi muhimu duniani na kwa kweli tunaipongeza kwa jinsi inavyotimiza majukumu yake ya kimataifa kwa kupitia mashirika mbali mbali ya kimataifa kama vile UNIDO (United Nations Industrial Development Organisation) na IAEA (International Atomic Energy Agency) ambalo kwetu Tanzania limetusaidia kuiboresha huduma ya mionzi kwenye Hospitali ya Ocean Road.”
Katika mazungumzo yake na Rais, Balozi Paulsen amesifia hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kubadilisha maisha ya Watanzania kwa njia za ubunifu zaidi.

“Tumekuwa tunafuatilia kwa makini na kwa karibu hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Serikali yake katika kuboresha uchumi kwa kutumia njia za ubunifu kama vile utaratibu mpya wa kuiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake kwa haraka zaidi ambao umeanzishwa karibuni. Tunakupongeza sana kwa kazi nzuri.”