RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete , Ijumaa, Julai 3, 2015, amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Argentina katika Tanzania, Bi. Bibiana Lucila Johnes, mwenye makazi yake Nairobi, Kenya. Katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Kikwete amemkaribisha Balozi Johnes katika Tanzania na kuomba balozi asaidie kushawishi wawekezaji wa Argentina katika sekta ya maendeleo ya mifugo na ngozi kuja kuwekeza katika Tanzania.
“Argentina ni gwiji duniani katika sekta ya maendeleo ya mifugo na ngozi na Tanzania inaweza kunufaika sanaa na uwekezaji na utaalamu kutoka kwenu kwa sababu Tanzania ina mifugo mingi ambayo faida yake inaweza kuongezwa sana kwa uwekezaji wa msingi.”
Wakati huo huo; rais Kikwete amepokea Hati za Utambulisho za Balozi mpya wa Qatar katika Tanzania, Abdallah Jassim Mohamed Al-Medady. Katika mazungumzo na Balozi Al Medady baada ya kupokea hati zake za utambulisho, Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itatafuta kufuata mfano mzuri wa Qatar katika matumizi mazuri ya mapato ya mauzo ya gesiasilia. Qatar ni moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa uzalishaji wa gesiasilia.
“Kama kuna ubalozi hapa nchini utakuwa muhimu sana kwetu kwa kadri tunavyojaribu kuanza uzalishaji wa gesiasilia nchini ni ule wa kwako, Mheshimiwa Balozi. Hivyo, usishangae tukipiga hodi kuomba ushauri kuhusu raslimali hii muhimu.”
Rais Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Qatar itaendelea kufanya kazi vizuri na Serikali mpya ambayo itaundwa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Baadhi yetu tutakuwa tunastaafu katika miezi michache ijayo na kubakia kama raia wa kawaida. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kufanya kazi na kuunga mkono Serikali ijayo kama mlivyotufanyia sisi. Tunawashukuru sana.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete ameagana na Balozi Nasri Salim Abu Jaish wa Palestina ambaye amemaliza muda wa utumishi wake katika Tanzania. Balozi Jaish ambaye alipata elimu yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada na mapambano ya Wapalestina kudai haki yao ya kuwa na taifa huru na linaloweza kujiendesha kiuchumi na kwa vigezo vingine vyote vya nchi huru.
Naye Rais Kikwete amemwambia Balozi Jaish kuwa msimamo wa Tanzania utaendelea kuwa ule ule kama ulivyoasisiwa mwaka 1967 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kufuatia Vita ya Siku Sita. Balozi Jaish amemwambia Rais Kikwete kuwa anahamishiwa Addis Ababa, Ethiopia ambako atakuwa Balozi wa Palestina katika Ethiopia na katika Makao Makuu ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU).
Vile vile, Rais Kikwete amekutana na kuzungumza na Balozi Martin Aduki, Mjumbe Maalum wa Rais wa Congo Brazzaville, Mheshimiwa Sassou Nguesso. Miongoni mwa mambo mengine, Mjumbe huyo maalum amewasilisha mwaliko wa kumwomba Rais Kikwete kuhudhuria mkutano maalum wa kujadili maendeleo ya mawasiliano ya digitali katika Afrika ambao utafanyika baadaye mwezi huu mjini Brazzaville. Marais wanane wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.