Rais Kikwete Apangua ‘Vigogo’ Jeshi la Polisi

DCP Thobias Andengenye  kapandishwa cheo kuwa Kamishna na kuteuliwa kuwa Kamishna wa Utawala na Utumishi..

DCP Thobias Andengenye kapandishwa cheo kuwa Kamishna na kuteuliwa kuwa Kamishna wa Utawala na Utumishi..


Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete amewapandisha vyeo Maofisa Wakuu wanne wa Jeshi la Polisi Tanzania na kufanya uteuzi wa nafasi za madaraka kufuatia mabadiliko ya muundo wa jeshi hilo kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florens Turuka waliopandishwa vyeo kuwa makamishna wa polisi (CP) ni pamoja na DCP Ernest Mangu, DCP Thobias Andengenye, DCP Abdulrahaman Kaniki na DCP Hamdan Omari Makame.

Taarifa hiyo imeonesha kuwa walioteuliwa nafasi za madaraka ni CP Clodwing Mtweve ambaye anakuwa Kamishna wa Fedha na Utaratibu wa Ugavi na Usafirishaji wa Watu na Vitu (Logistics), CP Paul Chagonja ambaye anakuwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo.

Wengine walioteuliwa ni CP Isaya Mungulu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya jinai (DCI)nafasi iliyoachwa wazi na Manumba, CP Mussa Ali Mussa ambaye ameteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Jamii.

Kwa mabadiliko hayo CP Hamdan Omari Makame ambaye anakuwa Kamishana wa Polisi, Zanzibar; CP Ernest Mangu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Jinai, CP Thobias Andengenye ambaye anakuwa Kamishna wa Utawala na Utumishi, huku CP Abdulrahman Kaniki anakuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Ushahidi wa Jinai na CP Abdulrahman Diwani ambaye anakuwa Naibu Mkurugenzi wa DCI. Katika mabadiliko hayo Rais pia amempandisha cheo SACP Athuman Diwani kuwa Naibu Kamishna wa Polisi.

Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kikwete amemteua Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Mbunge. Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, Desemba 3, 2013, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florens Turuka inasema kuwa uteuzi huo umeanza jana, Desemba 2, 2013. Dk. Asha-Rose Migiro ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Chama cha Mapinduzi.