Rais Kikwete Apangua Makatibu Wakuu na Manaibu

atibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu mabadiliko ya uongozi katika ngazi za juu za utendaji kazi Serikalini  kwenye  nafasi za makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika wizara mbalimbali.(Picha na Eleuteri Mangi -MAELEZO)

Na Magreth Kinabo, Maelezo – Dar es Salaam

RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya uongozi kwenye ngazi za juu za utendaji wa Serikali kwa nafasi za makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika wizara mbalimbali, ambapo wapo waliohamishwa, wataopangiwa kazi nyingine na wanaostaafu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. “Rais amefanya mabadiliko haya kwa lengo kuu la kuimarisha utendaji wa kazi za Serikali katika ngazi hizo za juu,” alisema Balozi Sefue.

Mabadiliko yaliyofanywa kwa upande wa makatibu wakuu ni kama ifuatavyo; Dk. Florens Turuka amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Joyce Mapunjo Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Jumanne Sagini amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi wa Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Wengine ni Dk. Servacius Likwalile amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, awali alikuwa Naibu Katibu Wizara ya Fedha, Dk. Patrick Makungu amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo, Alphayo Kitanda amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Dk. Shaaban Mwinjaka amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Dk.Uledi Mussa amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, awali alikuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Profesa Sifuni Mchome amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, awali alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.

Wanaofuata ni Charles Pallangyo amekuwa Katibu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri,  Anna Maembe amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, awali  alikuwa Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Sihaba  Nkinga amekuwa Katibu  Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo na  Sophia Kaduma amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Balozi Sefue aliongeza kwamba Katibu Mkuu aliyepewa uhamisho ni Peniel Lyimo ambaye anahamia Ofisi ya Rais – Ikulu kwenye ‘Presidential‘s Delivery Bureau’ kama Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo mwanzoni alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Makatibu wakuu watakaopangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Kijakazi Mtengwa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto na  Injia Omari Chambo aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.

Kwa upande wa Makatibu wanaostaafu ni Patrick Rutabanzibwa ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amestaafu kwa hiari. Aidha Balozi Sefue alisema Rais Kikwete pia amefanya uteuzi wa naibu makatibu wakuu wapya na kuwapa uhamisho baadhi yao. 

Alisema naibu makatibu wakuu wapya walioteuliwa ni Angelina Madete Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Regina Kikuli Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Zuberi Sumataba Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI- anayeshughulikia suala la elimu katika ngazi za Serikali za Mitaa, Edwin Kiliba Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu –  TAMISEMI.

Wengine Deodatus Mtasiwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI ambaye atashughulikia saula la afya upande wa  Serikali za Mitaa, Dk. Yamungu Kayandabila amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Adolf Mkenda Naibu Katibu Mkuu ya Fedha anayeshughulikia sera, Dorothy Mwanyika Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Fedha anayeshughulikia Fedha za Nje na Madeni.

Rose Shelukindo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Selassie  Mayunga Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Monica Mwamunyange Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Consolata Mgimba Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Naibu makatibu wakuu wengine ni Profesa Elisante ole Gabriel Laizer amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Armantius Msole Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Sefue aliwataja naibu makatibu wakuu waliopewa uhamisho kuwa ni John Mngondo ambaye amehamishiwa Wizara ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ametoka Wizara ya Uchukuzi katika nafasi hiyo, Selestine Gesimba amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii anatoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Injinia Ngosi Mwihava anahamia Wizara ya Nishati na Madini kutokea Ofisi ya Makamu wa Rais.

Wanaofuatia ni Maria Bilia amehamia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Nuru  Milao anahamia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.