RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete leo, Novemba Mosi, 2014, ameongoza waombolezaji kuaga mwili wa Meja Jenerali Aidan Isidori Mfuse kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Lugalo, mjini Dar Es Salaam. Meja Jenerali Mfuse ambaye nambari yake ya usajili wa Jeshi ilikuwa P1624 alifariki dunia Oktoba 29, 2014, katika Hospitali ya Apollo, nchini India, ambako alikuwa anatibiwa.
Rais Kikwete amewasili kwenye Hospitali ya Lugalo (GMH) kiasi cha saa tano asubuhi kujiunga na waombolezaji wengine akiwamo Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjmin William Mkapa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dk. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange. Meja Jenerali Aidan Isidori Mfuse alizaliwa Julai Mosi, mwaka 1948, mkoani Njombe na alipata uofisa wa Jeshi Desemba 23, mwaka 1972, alipopandishwa kuwa Luteni. Alistaafu Jeshi Juni 30 mwaka 2007 baada ya kuwa amelitumikia miaka 34, miezi minne na siku 13.
Katika salamu zake za rambirambi alizomtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange; “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Meja Jenerali Mstaafu, Aidan Isidore Mfuse kilichotokea katika Hospitali ya Appolo iliyoko nchini India alikopelekwa kwa matibabu. Kifo chake ni pigo kwa Taifa letu kwa vile, pamoja na kwamba alikuwa ameshastaafu, ushauri wake ulikuwa bado unahitajika ndani ya Utumishi wa Majeshi yetu”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Meja Jenerali Makunda alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Mwaka 1970. Alilitumikia Jeshi hilo kwa muda wa miaka 37 baada ya kupata mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kama zikiwamo nchi za India, Ghana na Kenya, na kutunukiwa Nishani kadhaa zikiwemo za Utumishi wa Muda Mrefu na Uliotukuka na Miaka 40 Nishani ya Muungano. Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Meja Jenerali Mstaafu, Aidan Isidore Mfuse kama Askari aliyekuwa na nidhamu na mwenye bidii ya kazi, sifa ambazo zililetea heshima kubwa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.
“Kwa kutambua sifa zake hizo na mchango wake mkubwa kwa Taifa, kifo cha Meja Jenerali Mfuse kimetuhuzunisha sote kama Taifa. Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia Salamu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wapiganaji Hodari wa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kupitia kwako naomba pia Salamu hizi ziwafikie Askari na Wapiganaji wote wa JWTZ kwa kumpoteza mwenzao”. Amewaomba wanafamilia wawe watulivu, wenye subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kifo cha mpendwa wao. Amewahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo.