Rais Kikwete aongeza muda wa kupokea majina ya wajumbe wa Katiba Mpya

Katiba ya Tanzania ya sasa

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, leo Machi 16, 2012, ameongeza muda wa kuwasilisha majina ya wanaopendekezwa kuwa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa muda wa siku saba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue sasa siku ya mwisho kuwasilisha majina hayo imeongezwa hadi Machi 23, 2012.

Rais alitoa mwaliko kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za dini, asasi za kiraia, jamii, taasisi na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana, kuwasilisha orodha ya majina ya watu wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume iliyotajwa hapo juu. Tarehe ya mwisho kuwasilisha orodha ya majina ilikuwa ni leo, Machi 16, 2012.

Taarifa ya Rais imedai licha ya idadi nzuri ya majina ambayo tayari yamewasilishwa, huenda bado yapo mapendekezo ambayo yametumwa kwa njia mbalimbali lakini yamechelewa kuzifikia ofisi za Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Inawezekana pia kwamba kuna watu ambao walitumwa na taasisi zao kutoka mikoani kuwasilisha mapendekezo hayo kwa mkono ambao pengine bado hawajafika. Aidha, inawezekana kuwa yapo mapendekezo mengine ambayo yametumwa kwa njia ya Posta na ambayo bado yapo njiani.”

Kwa kuzingatia yote haya na kwa uzito na umuhimu wa jambo lenyewe, Rais Kikwete, ameamua kuongeza muda wa kupokea mapendekezo kwa siku saba zaidi hadi tarehe 23 Machi, 2012. Kwa msingi huo, siku ya mwisho ya kuwasilisha orodha ya majina sasa itakuwa tarehe 23 Machi, 2012.

“Kwa wale ambao walichelewa kuandaa mapendekezo yao, wanaweza bado kutumia fursa hii ya kuongezwa kwa muda kuwasilisha mapendekezo yao kwa njia za haraka kama vile: njia ya mkono, kutumia nukushi na barua pepe. Mapendekezo yanayoletwa kwa nukushi na barua pepe yafuatiwe mara moja na nakala halisi.”

Kwa mujibu wa mwaliko uliotolewa na Rais wadau mbalimbali wanatakiwa kupendekeza majina ya watu wasiozidi watatu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika kifungu cha sita cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sifa hizo ni:-

Uzoefu katika kufanya mapitio ya Katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya Katiba, Sheria, Utawala, Uchumi, Fedha na Sayansi ya Jamii. Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii. Kama ilivyokuwa awali, mapendekezo ya majina ya wajumbe wa Tume ya Katiba yaletwe kwa:-