Rais Kikwete Aomboleza Vifo vya George Lindi na Hashim Sagaf

Marehemu, Hashim Sagaf

Marehemu, Hashim Sagaf

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha ghafla cha aliyekuwa msajili wa kwanza wa vyama vya siasa nchini, George Liundi kilichotokea juzi, Januari 12, 2014, nyumbani kwake Keko, mjini Dar Es Salaam.

Katika salamu zake za rambirambi ambazo alizituma usiku wa jana, Jumatatu, Januari 13, 2014, kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, Rais Kikwete amesema kuwa amepokea taarifa cha kifo cha Bwana Liundi kwa masikitiko na huzuni.

“Bwana Liundi alikuwa mtumishi mtiifu wa umma, alikuwa mchapakazi wa kuaminika na alikuwa mwandishi hodari wa sheria. Tutamkumbuka kama mtumishi mwadilifu na mwaminifu wa umma na mfano wa kuigwa wa utumishi bora,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi na kuongeza:
“Nakutumia wewe Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi salamu zangu za rambirambi, nikiungana nawe kuomboleza kifo cha Bwana Liundi.

Aidha, kupitia kwako nawatumia wanataaluma wote wa sheria nchini salamu nyingi za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzao.” Ameongeza: “Napenda vile vile kupitia kwako unifikishie pole nyingi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia wa Marehemu Liundi ukiwajulisha kuwa niko nao katika masikitiko na majonzi ya msiba huu mkubwa. Wajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira kuweza kuvuka kipindi hiki kigumu.

Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze peponi roho ya Marehemu George Liundi. Amen.”

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameomboleza kifo cha Diwani wa Kata ya Mchafukoge, Jijini Dar es Salaam na Mbunge wa zamani wa Dodoma Mjini, Hashim Sagaf kwa kumtumia Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas Masaburi na familia ya wafiwa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha diwani huyo.
Wakati huo huo; Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo cha Sagaf, ambacho kimetokea katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam na kuzikwa leo hii mjini Dar es Salaam.

“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha Mheshimiwa Sagaf ambaye nimejulishwa kuwa amepoteza maisha yake leo. Nilimfahamu Mheshimiwa Sagaf kwa miaka mingi. Alikuwa ni kiongozi hodari wa umma. Alikuwa raia mwaminifu kwa nchi yake na mzalendo wa kweli kweli ambaye aliitetea nchi yake na maslahi yake katika maisha yake yote. Alithibitisha sifa hizo katika maisha yake na katika nafasi zote za uongozi ambazo alizishikilia. Alikuwa mfano wa kuigwa katika utetezi wa nchi yetu na maslahi yake.”

“Nakutumia wewe Mheshimiwa Masaburi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, salamu za dhati ya moyo wangu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Sagaf. Aidha, kupitia kwako, naomba uniwasilishie salamu zangu za pole nyingi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia za Mheshimiwa Sagaf,” amesema Rais Kikwete katika rambirambi zake na kuongeza: “Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa wa kuondokewa na mhimili wa familia. Natambua uchungu wao na naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema poponi roho ya Mheshimiwa Hashim Sagaf. Amin.”