Rais Kikwete amzika Jenerali Mayunga Shinyanga

Rais Kikwete akisaini kitabu cha msiba wa Jenerali Mayunga.

Na Mwandishi Maalumu, Shinyanga

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete Agosti 12, 2011 aliongoza mamia ya waombolezaji kumzika Luteni Jenerali Silas Peter Mayunga kwenye makaburi ya Wasabato ya Unyanyembe mjini Maswa mkoani Shinyanga.
Jenerali Mayunga, shujaa wa Operesheni Chakaza ya kumung’oa Idi Amin baada ya kuwa ameivamia Tanzania mwaka 1978, alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Apollo ya mjini New Delhi, India ambako alikuwa anatibiwa. Alikuwa na umri wa miaka 71.
Jenerali Mayunga amezikwa kwa taratibu zote za Kanisa la SDA Church – Southern Conference (Kanisa la Wasabato) na zile za kijeshi ikiwa ni pamoja na mizinga 15 na gwaride la heshima la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Rais Kikwete ameungana na viongozi wengine mbalimbali wa kitaifa katika mazishi hayo. Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa, Waziri wa Ulinzi Hussein Mwinyi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Amina Masenza, wenyeviti wa CCM wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza, wabunge wa Mkoa Shinyanga akiwemo Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) Mheshimiwa Andrew Chenge, Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA) Mheshimiwa John Shibuda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davies Mwamunyange na viongozi wengine waandamizi wa jeshi na wapiganaji.
Rais Kikwete akiwa na mkewe Mama Salma Kikwete aliwasili makaburini majira ya saa 9: 56 mchana baada ya kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Shinyanga kwa ziara ya siku mbili ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mazishi hayo.
Mara baada ya Mheshimiwa Rais kuwasili makaburini, gwaride la jeshi lililobeba mwili wa marehemu liliingia makaburini kiasi cha saa 10:12 mchana na mwili wa marehemu uliteremshwa kaburini kiasi cha saa 10:30 kamili mchana.
Mjane wa marehemu na watoto wake walikuwa wa kwanza kuweka udongo kaburini akifuatiwa na Rais na Mama Salma, Lowassa, Mwinyi, Masenza, Jenerali Mwamunyange na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Luteni Jenerali Colleta Ivan ambaye baadaye aliwasomea waombolezaji salamu za rambirambi za Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuomboleza kifo cha Jenerali Mayunga.
Katika salamu zake, Rais Museveni ameelezea mchango wa Jenerali Mayunga katika Operesheni Chakaza akisema kuwa alikuwa ni Jenerali huyo ambaye alimpokea Museveni na wapiganaji wake 28 wa awali kwenye Shule ya Msingi ya Nyamiyanga mkoani Kagera Desemba 23, mwaka 1978.
“Wakati Kampala inatekwa kutoka mikononi mwa majeshi ya Idi Amin na kufikia hatua muhimu ya kuikomboa Uganda Aprili 11, 1979, askari wapiganaji katika kikosi hicho cha Waganda kilikuwa kimefikia wapiganaji 9,000 na yote hii ilikuwa kazi ya Jenerali Mayunga ambaye alitoa mchango mkubwa sana kuongeza askari hao kwa kiwango hicho kikubwa mno. Tumepotelewa na mpiganaji na kamanda hodari,” alisema Rais Museveni katika salamu zake.