RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuomboleza kifo cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eriya Kategaya kilichotokea Machi 2, 2013 katika Hospitali moja ya Nairobi, Kenya, alikokuwa anapata matibabu.
Katika salamu hizo za Machi 4, 2013, Rais Kikwete amemwambia Rais Museveni, “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Eriya Kategaya, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, ninatumia wewe salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako kwa wananchi wa Uganda na familia ya wafiwa.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nilimjua na kufanya kazi na marehemu Eriya Kategaya kwa zaidi ya miongo miwili. Nilimjua kuwa mtu makini, mzalendo wa kweli kweli wa nchi yake na bingwa hodari wa ushirikiano wa karibu zaidi wa Afrika Mashariki. Wananchi wa Uganda na eneo zima la Afrika Masariki limepotelewa na mtoto hodari na kiongozi mwerevu ambaye alichangia sana maendeleo na ustawi wa Jamhuri ya Uganda na Jumuia ya Afrika Mashariki.”
“Amefariki wakati uongozi wake ulipokuwa unahitajika zaidi. Hakuna shaka kuwa atakumbukwa daima kwa upendo na atakumbukwa kwa hamu na sisi sote, “ amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mawazo na sala zetu ziko na wewe Mheshimiwa Museveni, wananchi wa Uganda na familia ya wafiwa wakati huu mgumu wa maombolezo na huzuni. Tunamwomba Mwenyezi Mungi aiweke peponi pema roho ya Mheshimiwa Ertiya Kategaya. Amina.”