Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hajat Amina Mrisho kufuatia vifo vya watu 10 na wengine 19 kujeruhiwa kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea Septemba 14, 2011 katika kijiji cha Mwindu wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani. Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la Kampuni ya Grazia Safari’s kupinduka likitokea Songea kuelekea Dar es Salaam.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa leo, Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa, na kusikitishwa kwa Taifa kupoteza, kwa mara nyingine, roho za Watanzania 10 waliofariki kutokana na ajali hiyo ya basi la abiria.
“Naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hii mbaya. Nawahakikishia kwamba nipo pamoja na familia hizo katika kipindi chote cha maombolezo kwani msiba huu ni wetu sote,” alisema Kikwete katika taarifa hiyo.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azilaze pema peponi roho za marehemu wote. Aidha, amesema anawaombea kwa Mola wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia zao na kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Amesema kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani ambazo zimeendelea kulinyang’anya Taifa nguvukazi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, vyombo vyote vinavyohusika na usalama wa barabarani havina budi kusimamia kwa karibu mwenendo wa vyombo vya usafirishaji wa abiria ili kuepusha kutokea kwa ajali zaidi za barabarani.