Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kufuatia kifo cha Brigedia Jenerali Ally Abdallah Sinda kilichotokea ghafla jijini Dar-es-Salaam tarehe 17 Julai, 2011 asubuhi katika Hospitali ya Jeshi, Lugalo (521 KJ).
“Tumempoteza mpiganaji hodari katika ulinzi wa nchi yetu na pia katika kupigania afya za Watanzania mbalimbali waliofika katika hospitali yetu ya Jeshi na kupata huduma za kitabibu.” Rais ameeleza na kuongeza kuwa mchango wake mkubwa katika kulitumikia Jeshi na kulinda taifa letu kamwe hautasahaulika na tunamshukuru Mungu kwa mchango wake huo mkubwa. “Tunamwombea mapumziko mema na Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira, familia yake, ndugu na wanajeshi wenzake wakati huu wa msiba mkubwa, hatuna uwezo wa kuzuia kazi ya Mungu, ila kuzidi kumwombea mapumziko ya kheri milele”. Rais amemwandikia Jenerali Davis Mwamunyange na kumuomba amwakilishie rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu Brigedia Jenerali Sinda.
Wakati huo huo, Rais Kikwete pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia na wananchi wa Kagera kufuatia kifo cha Ndugu Daud Bakanyoma Simon Zimbihile aliyekuwa mbunge wa Jimbo lililokuwa likijulikana kama Ihangilo, na baadaye Muleba, ambalo sasa limegawanyika na kuwa Muleba Kaskazini na Kusini.
Marehemu Zimbihile amefariki dunia jana tarehe 18 Julai, 2011 kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu.
Marehemu Zimbihile aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Muleba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa.
Ameacha watoto watano na wajukuu kumi na moja.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2011