RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana kuomboleza kifo cha Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Emmanuel Mteming’ombe kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 19 Desemba, 2013 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa pumu na figo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa, Emmanuel Mteming’ombe kilichotokea tarehe 19 Desemba, 2013 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kutokana na ugonjwa wa pumu na figo”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Mteming’ombe, enzi za uhai wake, kama Kada Hodari, Mwaminifu na Mchapakazi wa Chama Cha Mapinduzi ambaye alipikwa vilivyo na Chama tangu alipokuwa na wadhifa wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Chuo cha Utabibu Songea, hadi alipoteuliwa kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma kabla ya kuhamishiwa katika Mkoa wa Iringa ambako mauti yamemkuta.
“Kwa hakika kifo cha Emmanuel Mteming’ombe kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa Wana-CCM, na kimesababisha pengo kubwa katika Chama chetu lisiloweza kuzibika kwa urahisi siyo tu katika Mkoa wa Iringa aliokuwa akiutumikia, bali Taifa kwa ujumla kwa vile mchango wake kwa CCM ulikuwa ndiyo kwanza unahitajika zaidi ili kukiimarisha na kukiendeleza zaidi Chama, na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi zaidi katika nchi yetu”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Abdulrahaman Kinana Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Kada muhimu katika Chama. Aidha natoa pole kwa Wana-CCM wote wa Mkoa wa Iringa na kwa kweli Wana-CCM kote nchini kwa kuondokewa na Kada mwenzao”.
Vilevile Rais Kikwete amemuomba Katibu Mkuu wa CCM kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Emmanuel Mteming’ombe kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili muhimu wa familia, huku akisisitiza kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.
Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Emmanuel Mteming’ombe, na anamuomba Mola awape wanafamilia, ndugu na jamaa za Marehemu nguvu na moyo wa uvumilivu ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na mpendwa wao.