Rais Kikwete Amtembelea Mzee Yusuf Mzimba Muhimbili

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali na kumpa pole Mzee` Yusuf Mzimba, mmoja wa wazee marufu wa Klabu ya Dar es salaam Young Africans (YANGA), ambaye amelezwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiuguza majeraha kufuatia kugongwa na BodaBoda wiki iliyopita Barabara ya Nyerere jijini Dar es salaam. Mzee Mzimba amevunjika mguu wa kushoto na kupata majeraha ya usoni na mikononi. Hadi jana hali yake ilikuwa inaendelea vyema na Rais Kikwete amempa pole nyingi kwa maumivu aliyoyapata na kumtakia apate nafuu ya haraka. PICHA NA IKULU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, leo Jumapili Machi 10, 2013 amemtembelea Mzee Yusuf Mzimba, mmoja wa wazee wa Klabu ya Dar es salaam Young Africans (YANGA), ambaye amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam, akiuguza majeraha kadhaa kufuatia kugongwa na pikipiki maarufu kama ‘Bodaboda’ wiki iliyopita katika barabara ya Nyerere.

Rais Kikwete, ambaye amewasili leo kutokea Afrika Kusini katika ziara ya kikazi ya siku tatu, amempa Mzee Mzimba pole na kumuombea apate nafuu ya haraka. Katika ajali hiyo Mzee Mzimba amevunjika mguu wa kushoto na kupata majeraha madogo usoni na mikononi. Kwa mujibu wa madaktari na wauguzi hali yake inaendelea vyema baada ya kutibiwa, ikiwa ni pamoja na kuvishwa Plaster of Paris (Piopio).

Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, IKULU.