RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini, Machi 7, 2015, kwenda Kigali, Rwanda kwa ziara ya siku moja nchini humo kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame.
Wakati akiwa Kigali, miongoni mwa mambo mengine, Rais Kikwete atahudhuria mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini – Northern Corridor Integration Projects unaofanyika leo katika Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Mkutano wa leo unatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo na mbali na Tanzania, nchi za Burundi na Sudan Kusini pia zimealikwa kuhudhuria mkutano huo.
Lengo la mkutano huo ni kujadili hatua za utekelezaji wa miradi mbali mbali iliyokubaliwa kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane wa namna hiyo uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana, 2014. Rais Kikwete atarejea nchini jioni ya leo baada ya kumalizika kwa mkutano huo.