RAIS Jakaya Kikwete Agosti 3, 2012 amempokea Rais wa Msumbiji Armando Emilio Guebuza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika(SADC).
Rais Guebuza amefika nchini kuhudhuria kikao cha siku moja cha nchi tatu ambazo zinaunda Chombo cha Siasa, Ulinzi na Usalama cha SADC (TROIKA) kinachofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 4, 2012, chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria ni Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Troika na Rais Joseph Kabila wa DRC.
Hiki ni kikao cha kwanza tangu Tanzania ichaguliwe kushika nafasi ya uenyekiti wa TROIKA katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za SADC kilichofanyika tarehe 16 -17 Agosti, 2012 nchini Msumbiji.
Nchi tatu za TROIKA ni Afrika Kusini, Namibia na Tanzania, ambaye ndiye Mwenyekiti. Kikao hiki ni cha mpango kazi wa TROIKA kwa mwaka mzima wa uenyekiti wa Tanzania.
Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mpango kazi huo na ambayo Tanzania imerithi kutoka kamati iliyomaliza muda wake ni pamoja na mgogoro wa Mashariki ya Congo DRC, mchakato wa Katiba na Uchaguzi wa Zimbabwe na suala la Madagascar.