RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufuatia taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe nchini, marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi ambaye alijulikana sana kwa jina la kisanii la Bi. Kidude aliyefariki dunia Aprili, 17, 2013 akiwa eneo la Bububu, Zanzibar kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Kisukari kwa muda mrefu.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe na Mwimbaji Mashuhuri wa Nyimbo za Mwambao hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi maarufu kwa jina la Bi Kidude aliyefariki Aprili 17, 2013 akiwa nyumbani kwake eneo la Bububu, Zanzibar kutokana na ugonjwa wa Kisukari”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu Bibi Fatma Binti Baraka enzi za uhai wake kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya nchi yetu katika nyanja za Sanaa na Utamaduni ambapo alimudu kuitangaza vyema nchi yetu kupitia kipaji chake cha uimbaji kwenye matamasha mbalimbali aliyowahi kuhudhuria na uimbaji wake kuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi waliowahi kuhudhuria matamasha hayo, kuyasikiliza kwenye Radio na kuyatazama kupitia matangazo ya Televisheni.
“Kwa hakika Fani ya Sanaa na Utamaduni imempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika sana katika kuinua zaidi kiwango cha uimbaji wa Muziki wa Mwambao ambao umejizolea sifa nyingi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza,
“Kufuatia taarifa hizo za kusikitisha, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wasanii nguli wa Muziki wa Mwambao hapa nchini”.
“Vilevile naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Bibi Fatma Baraka Hamisi kwa kupotelewa na mhimili madhubuti wa familia. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu. Amina”, amesema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete amewapa pole Wasanii wote hapa nchini ambao kwa hakika watakuwa wameguswa sana na kifo cha Bibi Fatma Baraka ambaye alichangia vilivyo katika kuitangaza sanaa kupitia uimbaji wa Muziki wa Mwambao. Amesema “kwa wao, njia bora ya kumuenzi Bi. Kidude ni kuendeleza zaidi sanaa ya uimbaji wa Muziki wa Mwambao na kuyaenzi yote mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu.”
Rais Kikwete amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Fatma Baraka kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.