Rais Kikwete Ameonyesha Mfano wa Mafanikio – Rais Lungu

kikwete

Rais wa Jamhuri ya Zambia, Edgar Chagwa Lungu amesema kuwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika maendeleo ya Tanzania na amani ya Bara la Afrika ni mambo yasiyotiliwa shaka tena, akitamani naye apate mafanikio kama Rais Kikwete.
Aidha, Rais Lungu amesema kuwa Rais Kikwete ameonyesha kiwango kikubwa na cha juu cha uongozi, ambacho kinathibitishwa na aina ya mafanikio ambayo ameyaleta katika miaka yote ya uongozi wake.
Rais Lungu alifagilia na kusisitiza mafanikio hayo ya Rais Kikwete na uongozi wake kwa nyakati mbili tofauti jana, Jumatano, Februari 25, 2015, katika siku ya kwanza ya ziara rasmi ya siku mbili ya Rais Kikwete nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais Lungu.
“Nina mengi ya kujifunza kutoka kwa Mheshimiwa Kikwete ambaye kama mnavyojua anajiandaa kumaliza muda wake wa uongozi. Mimi bado mpya kabisa katika uongozi wa juu na hivyo nina mengi ya kujifunza kutoka kwake kwa sababu amefanikiwa sana katika uongozi wa nchi yake, “ Rais Lungu aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa na Rais Kikwete baada ya viongozi hao wawili kumaliza mazungumzo rasmi kati yao.
Akizungumza wakati wa dhifa ya taifa ambayo Rais Lungu alimwandalia Rais Kikwete kwenye Hoteli ya Taj Pamodzi mjini Lusaka, Rais Lungu alirudia kumpongeza na kumsifia Rais Kikwete kwa uongozi bora.
“Umeonyesha uongozi wa kutukuka sana ambao unathibitishwa na mafanikio makubwa katika miaka yote ya urais wako. Umeimarisha, umesimamia na kudumisha utawala bora, umepanua sana uhuru wa kila aina katika Tanzania ukiwemo uhuru wa vyombo vya habari. Tunakupongeza kwa mafanikio hayo na baadhi yetu tunaoanza uongozi tunatamani sana kufuata nyayo zao,” alisema Rais Lungu na kuongeza:
“Mchango wako katika kusaka amani katika Bara la Afrika ni jambo la kupongezwa sana na ni chimbuko la heshima kwetu sote na kwa Bara letu lote. Mchango wako katika maendeleo ya Tanzania na Bara la Afrika ni mambo yasiyotiliwa shaka na yoyote. Ni matumaini yangu na nataka kufuata nyayo za uongozi wako.”
Wakati wa dhifa hiyo, Baba wa Taifa la Zambia, Mzee Kenneth Kaunda alikunwa mno na muziki wa Malaika uliokuwa unatumbuizwa na bendi moja kiasi cha kuingia uwanjani na kumkaribisha Rais Kikwete pamoja na Rais Lungu uwanjani na kwa pamoja wakasakata rumba.
Rais Kikwete ambaye alikuwa Zambia kwa ziara rasmi kutokana na mwaliko wa Rais Lungu anakuwa kiongozi wa kwanza wa nje kutembelea Zambia rasmi tokea Rais Lungu ashike madaraka ya kuongoza Zambia mwezi uliopita