JK awapa wamachinga milioni 10 Mwanza, amtembelea Mwita Kyaro

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na wawakilishi wa kundi moja la wachuuzi (machinga) wa jijini Mwanza ambao leo Januari 6, 2012 walikwenda Ikulu ndogo ya jiji hilo na kumweleza changamoto zinazowakabiri, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji pamoja na taaluma ya kufanyia biashara. Rais Kikwete ametoa milioni 10 kwa ajili yawamachinga hao kukopeshana mitaji. (Picha na Ikulu)

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewachangia wachuuzi wadogo wadogo wa mitaani (Wamachinga) wa mjini Mwanza sh. milioni 10, ili kuongeza nguvu katika mfuko wa kukopeshana wa wachuuzi hao.

Rais Kikwete ametoa uamuzi wa kuchangia mfuko huo wa uwezeshaji wa Wamachinga hao baada ya kusikiliza maelezo ya shughuli zao na jitihada zao za kuanzisha mfuko wenye raslimali za kutosha za kuwawezesha wanachama wa kikundi cha Wamachinga cha Mwanza kukopeshana kwa nia ya kuongeza mitaji ya kufanyia shughuli zao.

Akizungumza na viongozi wa Wamachinga hao waliokwenda kumwona katika Ikulu ndogo ya mjini Mwanza, Februari 6, 2012, Rais Kikwete amesema kuwa ni matarajio yake kuwa fedha hizo zitatumika vizuri na kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete wakimjulia hali Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali (mst) Ernest Mwita Kyaro jijini Mwanza asubuhi ya leo Januari 6, 2012. Jenerali mstaafu Kyaro, ambaye alikuwa mkuu wa majeshi katika serikali ya awamu ya kwanza, amefurahi na kumshukuru sana Rais Kikwete na mkewe kwa kutembelea. Picha na Ikulu.


“Mkiwezesha kunithibitishia kuwa fedha hizo zimetumika vizuri na kwa madhumuni yaliyokusudiwa basi tutaangalia jinsi gani ya kusaidia zaidi katika siku zijazo,” Rais Kikwete amewaabia Wamachinga hao katika mkutano ambao ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo.

Wakati huo huo, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Mwanza usiku wa jana alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa wazee wa Mkoa wa Mwanza.

Katika mazungumzo hayo, wazee hao chini ya Mwenyekiti wao wa muda, Mzee Charles Masakulangwa wamemweleza Rais Kikwete kuhusu mipango yao mbalimbali ukiwamo mradi wa ujenzi wa afya wa hospitali.