RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Januari 4, 2013, amekutana na kufanya mazungumzo na Mshauri wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa Luteni Jenerali Babacar Gaye.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Jenerali Gaye wamezungumzia hali ilivyo mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako wapiganaji waasi wa M23 wanakabiliana na Serikali ya nchi hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemweleza Jenerali Gaye jitihada za kumaliza mgogoro huo mashariki mwa Congo ambazo zimekuwa zinafanywa na viongozi wa Afrika kupitia taasisi mbili, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na International Conference on Great Lake Region (ICGLR). Rais Kikwete pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Miongoni mwa mambo ambayo yamekubaliwa na viongozi wa nchi hizo ni kuunda kikosi maalum cha askari ambacho kitakwenda DRC kujaribu kuleta amani katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Naye Jenerali Gaye amemweleza Rais Kikwete jinsi gani UN inavyoweza kushirikiana na nchi za Afrika jirani na DRC kukabiliana na mgogoro huo ambako kwa kipindi fulani mwaka jana, waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma.
Mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Kikwete, Jenerali Gaye ameondoka nchini kwenda Uganda ambako anatarajiwa kukutana na Rais Yoweri Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR.