Na Mwandishi Maalumu, Davos-Uswisi
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo mafupi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodafone, Vittorio Colao mjini Davos, Uswisi. Vodafone ndiyo wanahisa wakuu wa kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.
Colao ambaye pia anahudhuria mkutano unaojadili masuala ya kiuchumi duniani (WEF) mjini Davos kama ilivyo kwa Rais Kikwete walipata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo hayo katika Hoteli ya Sheraton Waldhuus.
Mazungumzo hayo yaligusia mahusiano ya Vodafone na Serikali ya Tanzania na watu wake hususan katika uwekezaji kwenye jamii kusaidia kukuza, kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii nchini ikiwa ni utekelezaji wa azma na malengo makuu ya Vodafone ya kuchangia kubadili maisha ya Watanzania.
Vodafone kupitia Vodacom Tanzania imekuwa ikiwekeza kiasi kikubwa cha fedha kusaidia na kuunga mkono miradi mbalimbali ya kijamii nchini ikiwemo maeneo makuu matano ya Elimu, Afya, Kuinua vipato vya wanawake, Mazingira na Michezo ili kuunga mkono juhudi za Serikali zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika mazungumzo hayo mafupi, Colao alimuhakikishia Rais Kikwete kwamba Vodafone itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya jamii Tanzania hususan katika maeneo ya afya na elimu ambayo yanauhusiano wa moja kwa moja na wa karibu katika kuiwezesha jamii kuondokana na changamoto ambazo zinaweza kuathiri maendeleo ya watu na hivyo kushindwa au kupunguza kasi ya kubadili maisha yao.