Rais Kikwete ‘Ajivunia’ Uhuru wa Habari Tanzania Mkutanoni

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akizungumza.

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akizungumza.


Na Mwandishi Maalum, New York
TANZANIA inatarajiwa kupata sheria ya Uhuru wa kupata Habari ifikapo Mwezi Februari, Mwaka 2015. Rais Jakaya Kikwete amesema hayo Septemba 24, 2014 jijini New York alipokuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano unaohusu Uwazi na ushirikiano kati ya serikali na jamii (Open Government Partnership-OGP).
Rais Kikwete amesema, rasimu ya muswaada wa Uhuru wa kupata Habari uko katika hatua ya mwisho ambapo wadau mbalimbali wanashauriana na kutoa maoni tayari kupelekwa bungeni.
“Muswaada huo unatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Mwezi Novemba mwaka huu, na kufikia Mwezi Februari mwakani sheria mpya ya kupata Habari itakua tayari,” amesema.
Mwezi Oktoba Mwaka 2013 katika mkutano wa OGP jijini London, Rais Kikwete alitangaza nia na ujasiri ulioko Serikalini kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na sheria ya Uhuru wa Habari.
Rais amesema, Uhuru wa Habari ni muhimu kwa wananchi kwa sababu “Ni haki yao ya msingi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu maisha yao” na kuongeza kuwa “Ni muhimu wananchi kujua serikali yao inafanya nini kwa niaba yao” amesisitiza.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Barack Obama wa Marekani amesema OGP ni ubia kati ya Serikali na Wananchi wake. “Hakuna nchi yenye
majibu yote kwa suala hili la Uwazi katika Serikali, tunahitaji kujifunza kutoka kwa kila mmoja” na kuongeza kuwa ni jambo jema kwa serikali kuimarisha ushirikiano na taasisi za kijamii.
Viongozi wengine waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na Indonesia , Afrika ya Kusini na Ufaransa. Rais Kikwete yuko jijini New York kuhudhuria Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ambapo pamoja na mambo mengine anahudhuria mikutano mingine yenye maslahi kwa Tanzania.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Bwana Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Elimu ambaye amemshukuru na kumsifu Rais Kikwete kwa kusimamia Elimu nchini Tanzania.
“Tunataka kukusaidia kufikia malengo ya milenia, tunajivunia mafanikio makubwa uliyoyapata katika elimu” amesema Bw. Brown katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na wabia wa maendeleo ambao kwa pamoja wanataka kusaidia Serikali katika kuleta maendeleo na kunyanyua zaidi kiwango cha Elimu nchini.
Wabia hao ni pamoja na Shirika la Global Education, Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wawakilishi wa Serikali ya Uingereza na Benki ya Dunia.
Wengine ni kutoka Global Business Coalition na Dubai CARES ambao kwa pamoja wanataka kuinua kiwango cha Elimu ya Msingi na Sekondari kwa kusaidia na kuchangia ili kuboresha zaidi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Tarehe 25 Septemba, 2014, Rais Kikwete atahutubia Baraza la Umoja wa Mataifa ambapo hotuba hiyo itaonekana moja kwa moja kupitia UN webcast.