Rais Kikwete afanya mazungumzo na wadau wa maendeleo

Rais Jakaya Kikwete akiwa na viongozi mbalimbali wanaohudhuria mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Uchumi Duniani wa World Economic Forum (WEF) Davos, Uswisi.

Na Mwandishi Maalumu, Davos

RAIS Jakaya Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa nchi na taasisi mbalimbali wakati wa siku ya pili ya Kongamano la Dunia – World Economic Forum katika mji wa Davos nchini Uswisi.
Rais Kikwete alianza siku kwa kukutana na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Mama Sadako Ogata, ambapo walizungumzia mambo mbalimbali ya maendeleo pamoja na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan, na kuishukuru kampuni hiyo kwa misaada ya kimaendeleo ambayo imekuwa ikitoa kwa muda mrefu.

Rais Kikwete alifanya mazungumzo ya faragha na Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kabla ya kuelekea ukumbi mkuu wa mikutano wa Davos ambako alishiriki katika majadiliano kuhusu maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi ya Afrika.

Viongozi wa Guinea, Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini walishiriki katika mjadala huo, ulioratibiwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Gordon Brown.

Baada ya hapo Rais Kikwete alionana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Bill and Melinda Gates Foundation, Bill Gates kuhusiana na umuhimu wa kutumia teknohama kwenye kuongeza kasi ya gurudumu la maendeleo katika kilimo, elimu na afya.

Rais kikwete pia alikutana na ujumbe kutoka Makao Makuu ya Kampuni ya Phillips ya Uholanzi, ambayo ni mojawapo ya mkampuni yanayoongoza katika uzalishaji wa vifaa vya elekroniki katika sekta ya afya na jamii.