Rais Kikwete afanya mazungumzo na mjumbe wa Rais wa Urusi

Rais Jakaya Kikwete akimsindikiza/akiagana na mjumbe maalumu wa Rais wa Urusi, Mikhail V. Margelov Ikulu jijini Dar es Salaam leo Januari 13, 2012. PICHA NA IKULU.

Na Mwandishi Maakumu

RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mikhail V. Margelov, Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ya Februari 13, 2012 Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemtaka mjumbe Maalum huyo kusaidia kushawishi makampuni zaidi ya Urusi kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete ametaka Tanzania na Urusi kuongeza ushirikiano wa kiuchumi katika nyanja mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua ambazo zitaongeza idadi ya watalii wa Urusi wanaotembelea Tanzania. Mwaka jana ni watalii 4,500 wa Urusi waliotembelea Tanzania.
Rais Kikwete na Margelov pia wamezungumzia masuala mbali mbali ya kimataifa, ya kanda ya Afrika na ya uhusiano kati ya Tanzania na Urusi.
Mjumbe Maalum huyo wa Medvedev anatembelea Tanzania ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda. Alianza ziara yake kwa kutembelea Zanzibar jana na atakuwa Kenya kesho.