Rais Kikwete Afanya Mazungumzo na Bosi wa ICC

Mwendeshaji Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uharifu (ICC), Bibi Fatou Bensouda


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Machi 2, 2013, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwendeshaji Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uharifu (ICC), Bibi Fatou Bensouda. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Bibi Fatou Bensouda amemshukuru Rais Kikwete kwa jinsi Tanzania na nchi nyingine za Afrika zimekuwa zinaunga mkono shughuli za ICC.

Bibi Bensouda amemwambia Rais Kikwete: “ICC imepata nguvu zaidi kwa sasa kutokana na jinsi Mahakama hiyo inavyoungwa mkono na nchi za Afrika. Kumbuka kuwa Bara la Afrika zinaunda idadi kubwa ya nchi wanachama wa ICC. Bara la Afrika lina wanachama 34 kati ya 122 wa ICC kwa sasa.”
Hata hivyo, Mwendeshaji Mashikata Mkuu huyo amesema kuwa ICC na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zinastahili kuongeza kiwango cha majadiliano na mawasiliano ili kuondoka hali ya kutoelewana mara nyingi bila sababu za msingi. Mama huyo pia ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono shughuli za ICC. “Kwa kweli, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi ilivyoeleza msimamo wake kuhusu masuala na shughuli mbali mbali za ICC na jinsi ambavyo imeendelea kuunga mkono ICC.”

Naye Rais Kikwete amemwambia Bibi Fatou Bensouda kuwa kuna wakati Afrika ilikuwa imefadhaishwa na msimamo wa ICC wa kuupuza maoni ya Afrika hasa kuhusu suala la Darfur katika Sudan ambako ICC ilikuwa inatafuta kumkamata Rais Omar El Bashir wa Sudan kwa matatizo ya Darfur bila kwanza kusikiliza maoni na msimamo wa Afrika kuhusu suala hilo na masuala mengine.

“Kuna wakati ilionekana kama ICC ilikuwa imeundwa kuwafukuzia viongozi wa Afrika tu. Hata pale ambako tulielezea maoni yetu kuhusu masuala mbali tulionekana kupuuzwa. Ni dhahiri kuwa hali hiyo haikujenga uhusiano mzuri kati ya Afrika na ICC lakini sasa hayo yameisha. Yaliyopita siyo ndwele,” Rais Kikwete amemwambia Bibi Bensouda.
Bibi ambaye ni raia wa Gambia, alichukua nafasi ya kuwa Mwendeshaji Mashitaka Mkuu wa ICC Desemba 12, 2011 na kabla ya hapo alikuwa Mshauri wa Kisheria na Mwendeshaji Mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uharifu ya Rwanda (ICTR) mjini Arusha.