Rais Kikwete Aendelea Kuzindua Miradi ya Barabara Nchini

Rais Jakaya Kikwete akizindua moja ya mradi wa barabara

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Novemba 5, 2012, amehudhuria sherehe kubwa za kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa barabara moja na kwenye sherehe za ufunguzi wa barabara nyingine iliyokamilika.

Sherehe hizo mbili zimefanyika kwenye Mkoa wa Singida ambako Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara yenye kilomita 89.3 kutoka Manyoni kupitia Itigi, Mkoani Singida, hadi Chaya, Mkoani Tabora. Aidha, Rais Kikwete amefungua rasmi Barabara ya Issuna-Manyoni ambayo ujenzi wake umekamilika kwa kujengwa na fedha za Serikali ya Tanzania bila mkopo wala mfadhili yoyote. Sherehe za uzinduzi wa barabara hiyo zimefanyika mjini Manyoni.

Katika sherehe za kuweka jiwe la msingi zilizofanyika mjini Itigi, Rais Kikwete aliungana na mamia kwa mamia ya wananchi kushuhudia kuanza kwa jitihada za kuunganisha mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma kwa barabara ya lami kupitia mjini Tabora kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania. Kwa sasa Mikoa ya Singida na Tabora umeunganishwa kwa lami kupitia Igunga, Mkoani Tabora.

Barabara hiyo ambayo iliahidiwa na Rais Kikwete wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 na iliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM inajengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 102 zote zikitolewa na Serikali ya Tanzania. Mhandisi Mshauri atalipwa Sh. bilioni 3.9 na Serikali tayari imetoa Sh. bilioni 25 kulipa fidia kwa wananchi ili kupitisha ujenzi wa barabara hiyo.

Ujenzi wa barabara hiyo ni mwanzo wa ujenzi wa barabara ambayo itatoka Chaya kwenda Nyahuha, Tabora mjini, Urambo, Kazimwaba hadi kwenye daraja la Mto Malagarasi Mkoani Kigoma hadi mjini Kigoma.
Akizungumza kwenye sherehe za shughuli hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli amesema kuwa Mkoa wa Singida ambao mwaka 2005 ulikuwa na barabara za lami zenye kilomita tatu tu sasa una barabara za lami zenye urefu wa kilomita 367.

Barabara ya Issuna-Manyoni ni sehemu ya Barabara ya Singida-Manyoni yenye urefu wa kilomita 117 na imegharimu Sh. bilioni 32.24 na kujengwa kwa miezi 36 baada ya mkadarasi wa kwanza kushindwa kumaliza barabara hiyo kutoka Singida hadi Manyoni mwaka 2007.

Akizungumza kwenye sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa P. Ole Kone amesema kuwa kumalizika kwa barabara hiyo kunaondoa kero iliyokuwa inawakumba wasafiri katika barabara hiyo kwa sababu ya kukwama kwa magari wakati wa mvua. Mwaka 2007, magari yalikwama na kusababisha msururu wa kilomita 14. Naye Waziri wa Ujenzi, John Magufuli amesema kuwa Tanzania ni moja ya nchi tano tu katika Afrika ambazo zinatumia bajeti yake ya Serikali kuchangia maendeleo ya nchi kwa kuwajengea wananchi barabara.