Rais Kikwete Aenda Afrika Kusini kwa Vikao Muhimu

Ndege ya Rais wa Tanzania

Ndege ya Rais wa Tanzania

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini mchana wa leo, Novemba 4, 2013, kwenda Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambako atahudhuria vikao viwili muhimu vya Wakuu wa Nchi za Afrika.

Katika kikao cha kwanza, Rais Kikwete ataungana na wakuu wa nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na wakuu wa nchi za Umoja wa Maziwa Makuu (ICGLR) kujadili hali ya usalama katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mkutano wa dharura ulioitishwa kujadili suala hilo.

Mkutano huo utafuatiwa na kikao cha viongozi wa Afrika kujadili uundwaji wa kikosi cha muda cha askari cha kupambana na migogoro mbali mbali ya kijeshi katika Afrika – African Capacity for Immediate Response to Crises (ACIRC).

Kufanyika kwa mkutano kuhusu ACIRC kunafuatia maamuzi ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) waliokubaliana katika kikao chao mwezi Mei, mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia kuundwa kwa jeshi la kukabiliana na mizozo na migogoro ya kijeshi katika Afrika.

Kikao hicho cha kwanza kuhusu suala hilo ni mwanzo wa kutafuta kuundwa kwa vikosi vya jeshi vya African Standby Force (ASF) na Rapid Deployment Capacity (RDC).