RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete yuko nchini Afrika Kusini ambako atahudhuria mikutano miwili muhimu.
Rais Kikwete ambaye ameondoka nchini asubuhi ya Ijumaa, Machi 8, 2013 na akiwa nchini humo anatarajiwa kuhuduria Mkutano wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Vyama vingine ambavyo vilitarajiwa kushiriki mkutano huo ni vyama tawala vya Mozambique, Namibia, Afrika Kusini na chama cha ZANU-PF cha Zimbabwe. Jumamosi ya Machi 9, 2013, Rais Kikwete atahudhuria Mkutano wa Asasi Maalum ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo yeye ndiye mwenyekiti wake.
Asasi hiyo inatarajia kujadili maendeleo ya hali ya kisiasa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe na Madagascar. Rais Kikwete na ujumbe wake atarejea nchini baada ya kumalizika kikao hicho.