RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, a Jakaya Mrisho Kikwete ameongoza harambee ambayo ilifanyika Alhamisi, Machi 14, 2013, iliyowezesha kuchangiwa kwa kiasi cha Sh. Milioni 255 kwa ajili ya ujenzi wa Parokia mpya ya Kanisa Katoliki la Kigurunyembe katika Jimbo Katoliki la Mogororo.
Kati ya Sh. 255, 085, 610 zilizochangwa na waumini wa Kanisa hilo na dini nyingine nchini, wafanyabiashara, wabunge wa Mkoa wa Morogoro, wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, viongozi wa Kanisa Katoliki lenyewe, wananchi wa kawaida, viongozi wa Mashirika ya Umma na binafsi na taasisi nyingine za Serikali, kiasi cha Sh.73, 705, 610 zilichangwa taslimu kwenye hafla hiyo.
Kiasi kilichobakia cha Sh. 155, 380, 000 zimetolewa kama ahadi na wachagiaji mbali mbali. Rais Kikwete aliwaambia washiriki wa uchagiaji huo kuwa naye atatoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hilo na kuwa mchango wake utaingizwa katika akaunti ya ujenzi Jumanne ijayo.
Aidha kiasi hicho cha Sh. Milioni 255 ni pamoja na ahadi ya mabati 450 yenye thamani ya Sh. Milioni 16 ambayo imetolewa na mfanyabiashara wa Dar es salaam Bwana Bubash Patel na michango ya saruji na mchanga iliyotolewa na waumini wengine katika hafla hiyo.
Rais Kikwete alifanikisha lengo hilo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uchangiaji wa fedha za ujenzi wa kanisa jipya la parokia ya Kigurunyembe, mjini Morogoro iliyofanyika jana usiku kwenye Bwalo la Jeshi la Magadu Officer’s Club, nje tu ya mji wa morogoro.
Kanisa hilo jipya linalojengwa katika eneo tofauti na Parokia ya sasa ya Kigurunyembe limekadiriwa kugharimu kiasi cha Sh. Milioni 600 ambazo kati ya hizo tayari waumini wa Kanisa hilo walikwishachangia kiasi cha Sh. Milioni 130 kabla ya jana usiku.
Akimkaribisha Rais Kikwete pamoja na wageni wengine katika halfa hiyo ya uchangiaji wa ujenzi wa parokia hiyo, Askofu wa Jimbo la Morogoro, Baba Askofu Telesphory Mgude alisema kuwa katika uchagiaji wa jana usiku Jimbo la Morogoro lilikuwa limepanga kupata kiasi cha Sh. Milioni 200.
Askofu Mgude alisema kuwa Jimbo Katoliki Morogoro limeamua kujenga Parokia ya Kigurunyembe katika sehemu nyingine ya eneo hilo hilo la Kigurunyembe kwa sababu parokia ya sasa ya Kigurunyembe haina nafasi iliyobakia baada ya Serikali kutaifisha Chuo cha Ualimu cha Kigurunyembe kilichoko kwenye eneo la parokia ya sasa katika miaka ya 1960.
Askofu Mgude alimwambia Rais kuwa Parokia mpya inajengwa katika eneo jipya ambayo ardhi yake ilitolewa bure na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mogogoro, Marehemu Anselm Lyanda mwaka 2005.
Mbali na uchagiaji wa moja kwa moja, kiasi kikubwa cha fedha pia kilipatikana kwa kuuza kwa njia ya mnada sanamu tatu za Bikira Maria, zikiwamo za Bikira Maria wa Msaada na Bikira Maria Mkingiwa wa Dhambi ya Asili ambazo zote kwa pamoja zimeingiza Sh. milioni 4.1.
Aidha, ulikuwepo upigaji mnada wa keki ambayo ilinunuliwa kwa jumla ya Sh. Milioni 2.8 ambayo alikabidhiwa Rais Kikwete ambaye naye akiwakabidhi masista wa Kanisa Katoliki akiwaomba waikabidhi kwa watoto yatima nao wanufaike na matunda ya uchangiaji huo.