RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Oktoba 21, 2014, anaanza ziara rasmi ya siku sita katika Jamhuri ya Watu wa China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping, ikiwa ni ziara yake ya pili nchini humo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Baada ya China, Rais Kikwete atafanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Vietnam kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo.
Wakati wa ziara yake nchini China, Rais Kikwete ambaye aliondoka nchini, Oktoba 20, 2014, atatembelea majimbo matatu ya nchi hiyo, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa China, atashuhudia utiaji saini mikataba muhimu ya shughuli za maendeleo, atatunukiwa shahada za heshima na atashiriki katika sherehe za miaka 50 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na China.
Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Xi Jinping; Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Zhang Dejiang. Rais Kikwete pia atashuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maendeleo ya Tanzania ambayo inasaidiwa ama inagharimiwa na fedha kutoka China na pia atakutana kwa mazungumzo na wakuu wa taasisi muhimu zinazogharimia baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo katika Tanzania zikiwamo China-Africa Development Fund (CADB) na China Development Bank (CDB).
Akiwa Beijing, Rais Kikwete atakutana na Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika China, atafungua Mkutano wa Tatu wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na China na atazindua rasmi Kijiji cha Kiafrika. Aidha, Rais Kikwete atatunukiwa uprofesa wa heshima na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China cha China Agricultural University na Chuo Kikuu cha East China Normal University na pia atakuwa mwenyeji wa hafla maalum ya kusherehekea miaka 50 ya uhusiano wa kibalozi kati ya Tanzania na China. Uhusiano huo ulitimiza miaka 50, Aprili 26, mwaka huu, siku ambako Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ilitimiza miaka 50 ya kuzaliwa kwake.
Baada ya kumaliza ziara yake Beijing, Rais Kikwete atatembelea Jimbo la Jinan ambako atashuhudia maonyesho rasmi ya kijeshi ya Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China la Chinese People’s Liberation Army (PLA) lililoandaliwa rasmi kwa heshima yake. Hiyo itakuwa mara ya kwanza katika historia kwa heshima ya namna hiyo kutolewa kwa kiongozi wa nchi yoyote duniani, nje ya China.
Akiwa Jimbo la Jinan, Rais Kikwete pia atakutana na viongozi wa Jimbo hilo na pia atakutana kwa mazungumzo na madaktari wa Kichina ambao wamefanya kazi katika Tanzania katika miaka 50 iliyopita. Baada ya Jimbo la Jinan, Rais Kikwete atakwenda Jimbo la Shenzhen ambako atatembelea makao makuu ya taasisi na makampuni makubwa ya China ya Shenzhen Economic Zones Authority, China Merchants Holdings International (CMHI), Huawei na ZTE. Shenzhen ndiko Watanzania wengi wanaonunua bidhaa kutoka China hufanyia biashara zao. Mara ya mwisho, Rais Kikwete alitembelea China mwaka 2008 wakati alipoliwakilisha Bara la Afrika katika Mkutano wa Kwanza wa China-Afrika katika nafasi yake wakati huo kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).