Rais Kikwete Aanza Ziara Katika Mkoa Mpya wa Simiyu

Rais Jakaya Kikwete katika uwanja wa ndege Mwanza.

Rais Jakaya Kikwete katika uwanja wa ndege Mwanza.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Mwanza, Novemba 27, 2013, tayari kuanza ziara ya kikazi ya Mkoa mpya wa Simiyu. Rais Kikwete ataondoka mjini Mwanza asubuhi ya, Jumatano, kuingia Mkoa wa Simiyu na miongoni mwa shughuli zake itakuwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Lamadi kwa kiwango cha lami. Jiwe hilo la msingi litawekwa katika eneo la Old Maswa.

Baada ya hapo, Rais Kikwete atazindua mradi wa kusambaza umeme vijijini katika eneo la Nkololo kabla ya kuweka jiwa la msingi kwenye ujenzi wa Benki ya Wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Rais Kikwete ambaye atakuwa mkoani Simiyu kwa siku tano kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo atamaliza siku ya kesho kwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa Mkoa wa Simiyu katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Sabasaba mjini Bariadi.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa minne iliyoanzishwa na Rais Kikwete mwaka jana na unaundwa na maeneo yaliyokuwa Wilaya za Maswa na Bariadi katika Mkoa wa Shinyanga na Jimbo la Uchaguzi la Busega lililokuwa katika Mkoa wa Mwanza.