Rais Kikwete Aaanza Kuaga Watanzania Tanga

Rais wa Tanzania, Jakaya  Kikwete.

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete amewashukuru wananchi wa Tanga kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake hali iliyomwezesha kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo. Rais Kikwete amesema hayo katika Uwanja wa Mkwakwani Mjini TANGA tarehe 3 Augusti, 2015 wakati akiwaaga rasmi wananchi wa Tanga.

“Naungana nanyi kujipongeza kwa hatua za maendeleo tulizopiga katika kipindi cha miaka 10. Sote tunaona na kukiri kwa vinywa vyetu kuwa Tanga ya leo si ile ya miaka 10 iliyopita” Amesema Rais Kikwete

Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika mkoa wa Tanga katika kipindi chake cha uongozi wa miaka 10 kuwa ni ongezeko maradufu la pato la mtu kutoka shilingi 537,277/= mwaka 2005 hadi kufikia shilingi 1,187,044 mwaka 2013. Katika sekta ya Elimu Rais Kikwete amesema idadi ya vyumba vya madarasa ya awali vimeongezeka kutoka 127 hadi 418, shule za msingi zimeongezeka kutoka 3,943 hadi kufikia 8,821 na sekondari zimeongezeka kutoka 671 hadi kufikia 3,171.

Mafanikio mengine katika sekta ya elimu mkoani Tanga ni pamoja na kuongezeka kwa nyumba za walimu wa shule za msingi kutoka 597 hadi 1,883 na nyumba za walimu wa sekondari zimeongezeka kutoka 154 hadi kufikia 610 hivi sasa. Idadi ya walimu wa shule za msingi pia imeongezeka kutoka 1,807 hadi kufikia 7,256 wakati shule za sekondari zimeongezeka kutoka 772 hadi kufikia 5,193. Katika sekta ya afya Rais Kikwete amesema pamoja na kuiboresha na kuipandisha hadhi hospitali ya mkoa ya Bombo ambayo sasa ni hospitali ya Rufaa, zahanati zimeongezwa kutoka 146 hadi kufikia 263, vituo vya afya vimeongezeka kutoka 18 hadi kufikia 43.

Aidha amezungumzia mafanikio katika uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa vijijini Mkoani Tanga ambapo sasa wanavijiji 926,345 wanapata maji safi na salama kati ya 1,650,873 sawa na asilimia 56.3 ilihali Tanga Mjini asilimia 96 wanapata maji safi na salama na wanayapata jirani na makazi yao. Kwa upande wa Umeme, Rais Kikwete amesema serikali imeongeza upatikanaji wa umeme kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa kilometa 430.1 za umeme wa msongo mkubwa na kilometa 393 za umeme wa msongo mdogo na kuweka transfoma 126 kwenye wilaya za Korogwe, Lushoto na Handeni. Rais Kikwete ameongeza kuwa Serikali bado inaendelea na juhudi za kuboresha upatikanaji wa umeme.

“Tunafanya hivyo pia katika awamu ya pili kwa kujenga km 246.5 za umeme wa msongo mkubwa na km 177.5 za umeme wa msongo mdogo na uwekaji wa transfoma 86 katika wilaya za Muheza, Mkinga, Tanga na Pangani” Rais ameeleza na kuongeza kuwa

“Kutokana na juhudi hizo, tumepata mafanikio makubwa katika usambazaji umeme vijijini. Sasa vijiji 469 vimefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na vijiji 118 mwaka 2005 na hivyo kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma ya umeme kutoka asilimia 11.04 mwaka 2005 hadi asilimia 60.54 mwaka 2011”.

Rais pia amezungumzia sekta ya barabara mkoani Tanga kwa kueleza kuwa Mkoa umejengewa barabara muhimu kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara ya Mkata – Korogwe kupitia Handeni yenye kilometa 125 na Tanga – Hororo yenye kilometa 65.

Hata hivyo amesema serikali inaendelea na matayarisho ya ujenzi wa barabara nyingine za lami zikiwemo za Kibrashi- Songea, Soni – Bwembera – Dindira – Kwashemshi na barabara ya Handeni – Turiani – Kibirashi – Kondoa yenye urefu wa kilometa 460

“Tunaendelea na matayarisho ya ujenzi wa barabara za lami za Kibrashi hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Songe, Soni-Bwembera-Dindira-Kwashemshi kule Wilayani Lushoto, na ile barabara ya Handeni-Turiani-Kibirashi-Kondoa (km 460)” Rais amefafanua na kuwaeleza wananchi kuwa

“Mipango ya barabara hizi imeiva tayari kwa kujengwa. Tunaendelea pia kutafuta fedha kwa ajili ya barabara ya lami ya Tanga-Pangani-Bagamoyo na ujenzi wa daraja la Mligazi linalounganisha Wilaya ya Handeni (Tanga) na Miono (Pwani)”.

Kuhusu bandari ya Tanga na Reli, Rais Kikwete amesema juhudi zinafanyika kuirejesha Tanga katika umaarufu wake.

“Katika kuirejesha Tanga katika umaarufu wake wa zamani, tunafanya jitihada za kuimarisha bandari ya Tanga na reli ya kaskazini ya Tanga-Arusha-Musoma. Kwa kufanya haya viwanda vitarudi Tanga” amesema.

Rais amesema serikali imeamua kuifanya bandari ya Tanga kuwa bandari ya pili ya kupakulia mafuta yanayonunuliwa kwa pamoja yaani Bulk Procument System kuanzia Julai 2015 uamuzi ambao utafuatiwa na kujenga na kupanua bandari ya Tanga ili iweze kupokea meli kubwa zaidi.

Rais Kikwete pia amezungumzia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu kuwa yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na zoezi la uandikishaji wapiga kura lakini akawasihi watanzania kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mapema akizungumza kabla ya Rais Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Magalula Said Magalula amesema wananchi wa Tanga wanamshukuru Rais kwa maendeleo makubwa waliyoyapata katika kipindi cha uongozi wake.

Hata hivyo Magalula amemuomba Rais Kikwete amsisitizie Rais ajae kuendeleza juhudi kubwa zilizofanywa katika kipindi chake ikiwemo kuendeleza bandari ya Tanga, upanuzi wa barabara za lami na Reli pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanga Sheikh Mzee Makalo, amemshukuru Rais Kikwete kwa kuuwezesha mkoa wa Tanga kupata mabadiliko makubwa ya kimaendeleo na akasisitiza kuwa sio sahihi kwa mtu yeyote kudai hakuna maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Rais Jakaya Kikwete amesihi watanzania kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha vyanzo vya ajali vinakomeshwa ili kunusuru maisha ya watu ambayo hupotea kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika. Ameyasema wakati akifungua sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani zilizofanyika katika uwanja Tangamano Mjini.

Rais Kikwete amesema asilimia 56 ya ajali zote zinazotokea zinasababishwa na ukosefu wa umakini wa madereva na kwamba endapo madereva watatekeleza wajibu wao wa kuwa makini ajali hizo zinaweza kuepukika. Halikadhalika amesema endapo kila mwananchi atatimiza wajibu wake wa kukemea na kutoa taarifa katika vyombo husika dhidi ya vitendo vya uvunjaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani ajali hizo zitapungua.

Amebainisha kuwa kati ya mwaka 2010 na mwaka 2014 watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na watu 96, 708 walijeruhiwa, idadi ambayo inakaribia idadi ya watoto wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Malaria na kusisitiza kuwa idadi hiyo inaweza kuepukika.

“Hivi sasa idadi ya majeruhi wa pikipiki pekee ni kubwa kiasi kwamba wakati wagonjwa wa malaria wanapungua mawodini, majeruhi wa pikipiki wanaongezeka”

Rais Kikwete amewataka watumiaji wa barabara hususani madereva kuepuka uendeshaji wa mwendo kasi na kutoyapita magari mengine bila tahadhari kwa kuwa hivyo ndivyo vimekua vyanzo vikubwa vya ajali. Ameagiza kuweka matuta ya kudhibiti mwendo kasi katika maeneo yote yenye makazi ya watu ili kukabiliana na vifo vinavyosababishwa na madereva wanaoendesha mwendo mkali katika maeneo ya makazi ya watu. Aidha Rais Kikwete amelitaka jeshi la polisi kuweka kamera za kurekodi mwendo kasi wa magari barabarani badala ya kutumia askari.

“Mkitumia kamera kila atakayezidisha mwendo mtamkamata, lakini kwa kutumia askari mnatoa mianya ya baadhi ya watu kuendesha mwendo mkali na wanapokamatwa hawachukuliwi hatua”

Pamoja na kutaka polisi wafikirie kutumia kamera katika kukabiliana na ukikwaji wa sheria za usalama barabarani Rais Kikwete pia ametaka leseni za madereva wanaokamatwa kutokana na kuvunja sheria za usalama barabarani zianze kuwekwa alama ambazo ambazo hatimaye zitamwondolea dereva sifa ya kuendelea kuendesha gari.

“Mkifanya hayo ndio mtakua mnakwenda na wakati” Alisema Rais Kikwete

Mapema akitoa taarifa ya Baraza la Usalama barabarani Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Kamishna Msaidizi Mohamed Mpinga amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali yake katika ujenzi wa barabara hali iliyosaidia kupungua kwa ajali za barabarani ambazo zimekua zikisababisha vifo, majeruhi na watu kupata ulemavu. Pamoja na kutoa pongezi hizo Kamanda Mpinga pia amemuhakikishia Rais Kikwete kuwa Baraza hilo litaongeza juhudi za kukabiliana na vyanzo vya ajali vikiwemo uendeshaji wa mwendo kasi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula amesema mkoa huo umefanikiwa kupunguza madhara yatokanayo na ajali za barabarani ambapo vifo vimepungu kutoka 219 mwaka 2013 hadi kufikia vifo 144 mwaka 2014 na vifo 68 mwaka huu. Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la usalama barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Pereira Ame Silima amesema baraza hilo linaendelea kushauriana na serikali ili kuifanyia marekebisho sheria inayounda baraza hilo ili liweze kupata bajeti ya kuendesha shughuli zake.

WAKATI HUO HUO; Rais Jakaya Kikwete amesihi watanzania kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha vyanzo vya ajali vinakomeshwa ili kunusuru maisha ya watu ambayo hupotea kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika. Ameyasema wakati akifungua sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani zilizofanyika katika uwanja Tangamano Mjini.

Rais Kikwete amesema asilimia 56 ya ajali zote zinazotokea zinasababishwa na ukosefu wa umakini wa madereva na kwamba endapo madereva watatekeleza wajibu wao wa kuwa makini ajali hizo zinaweza kuepukika. Halikadhalika amesema endapo kila mwananchi atatimiza wajibu wake wa kukemea na kutoa taarifa katika vyombo husika dhidi ya vitendo vya uvunjaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani ajali hizo zitapungua. Amebainisha kuwa kati ya mwaka 2010 na mwaka 2014 watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na watu 96, 708 walijeruhiwa, idadi ambayo inakaribia idadi ya watoto wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Malaria na kusisitiza kuwa idadi hiyo inaweza kuepukika.