Rais Kenyatta Aahidi Kutimiza Matakwa ya WADA

Kenyan-President-Uhuru-Kenyatta-

Kenya itatimiza muda wa mwisho wa mwezi Mei kufuata mfumo wa shirika linalopambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli, WADA na kuepuka vikwazo

Vikwazo hivyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya Rio. Akizungumza katika hafla ya chai ya asubuhi aliyowaandalia wanariadha watakaoshiriki katika mbio ndefu, marathon na mbio za dunia za nusu marathon ikulu mjini Nairobi, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema serikali yake imeupa mswada huo umuhimu na anaufuatilia kwa karibu.

Ifikapo mwishoni mwa juma, mswada wa kupambana na madawa hayo, utakuwa umepitishwa na bunge na nitautia saini kuwa sheria ili kusiwe na kisingizio cha kuinyima timu yetu kushiriki katika michezo ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro mwezi Agusti, amesema.

“Tunafahamu kuna watu wanaotafuta visingizio kuhakikisha kwamba Kenya haishiriki katika Olimpiki. Hatutawapa nafasi hiyo” alinukuliwa akisema katika taarifa rasmi ya serikali.

Kenya imepatiwa muda wa nyongeza wa mwezi mmoja hadi Aprili 7 kufuata mfumo wa WADA ama itakabiliwa na vikwazo ambavyo ni pamoja na kupigwa marufuku kushiriki michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka huu.

Chanzo:dwswahili