RAIS wa Marekani Donald Trump ameanza kutia saini maagizo ya rais, baadhi yake yakiwa ni ya kubadili yale yalioafikiwa na mtangulizi wake Barak Obama. Muda mfupi baada ya kukagua gwaride la kuapishwa kwake, Bw Trump, alitia amri ya serikali, kupunguza mzigo wa kiuchumi kwa taifa, unaotokana na gharama za kufadhili bima ya matibabu ya bei nafuu inayofahamika kama Obamacare, ambayo Trump aliahidi kufanyia marekebisho.
Trump pia ametia saini amri ya kuwaidhinisha mawaziri wake wapya wa Ulinzi na usalama wa kitaifa ambao uteuzi wao umepitishwa na bunge la seneti. Utawala wa Trump pia umeaanza kufanyia marekebisho mtandao wa kijamii wa Ikulu ya White House kwa kuweka masuala yatakayopatiwa kipaumbele na uongozi huo mpya.
Donald Trump, Rais wa Marekani, ni tajiri anayemiliki majumba mengi na ambaye amekuwa mtangazaji wa kipindi cha maisha ya uhalisia kwenye runinga. Amekuwa mtu anayeangazia sana ushindi katika maisha yake na alikuwa tangu mwanzo amesema ni lazima afanikiwe katika kupata tuzo kuu duniani, kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Kwa wafuasi wake, ndiye anayeweza kuleta ufanisi kwa Marekani. Kwao, huyu ni tajiri shupavu anayeweza kusuluhisha matatizo yote ya nchi ambayo wanahisi yameshusha hadhi ya Marekani duniani. Wengi wao ni raia wa Marekani wafanyikazi hasa wenye asili ya Kizungu na walio na maisha ya kadri.
Hata hivyo kwa wakosoaji wake, walisema huyu ni mbaguzi na mfitini, mfidhuli mkubwa ambaye angepokeza ushindi kwa Hillary Clinton au kuitumbukiza dunia kwenye janga kubwa. Walinoa kwa hilo la kwanza kwani alimshinda Bi Clinton kwa urahisi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Novemba.
-BBC