Rais Dk Shein Awashangaa Wanaobeza Muungano

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, akipanda Mti mbele ya Tawi la CCM Fumba, baada ya kuweka jiwe la Msngi Tawi hilo akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi Wilaya ya CCM Dimani Mkoa wa Magharibi Unguja.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Makamo Mwenyekiti wa CCM  Zanzibar, akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tawi la CCM Fumba Abdalla Mohamed Hassan, alipotembelea sehemu za Ofisi za Tawi hilo baada ya kuweka jiwe la msingi akiwa katika ziara ya kumarisha Chama. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewashaangaa wanaoubeza Muungano wa Tanzania na kueleza kuwa wengi wa hao wamepata nyadhifa mbali mbali ndani ya Muungano huo.
 
Dk. Shein aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika ziara yake kwenye Mkoa wa Kichama wa Magharibi Unguja. Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa Muunganao wa Tanzania umewanufaisha watu wengi wakiwemo wale waliopata nyadhifa serikali ambao hivi leo wamekuwa wakiubeza Muungano huo bila ya sababu za msingi.
 
“Wengi wamepata vyeo ndani ya Muungano huu…. halafu leo anatokea mtu anaubeza Muungano huo huo  kwa kweli tutamshangaa”,alisema Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar.
 
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa si jambo la busara kuubeza Mungano wa Tanzania kwani umeweza kuleta mafanikio makubwa hapa nchini. Kutokana na umuhimu huo Makamu Mwenyekiti Zanzibar aliwataka WanaCCM kuuendeleza na kuuenzi Muungano huo ambao unatimiza miaka 49 tokea kuasisiwa kwake.
 
Katika kutambua hilo na kueleza ukweli Dk. Shein alisisitiza kuwa hakuna haja ya kutafuta maneno kwani kwani CCM inatambua kuwa Muungano uliopo ni wa Serikali mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na si vyenginevyo.
 
Alieleza kuwa CCM itaendelea kuudumisha Muungano huo wa Serikali mbili kwani ndio inaoutambua na ndio ulioasisiwa na waasisi wa Muungano huo hayati Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
 
Sambamba na hailo, Dk. Shein alieleza kuwa akiwa yeye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea kuuimarisha na kuuenzi Muungano huo sanjari na kuyalinda na kuyadumisha Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
 
Makamu Mwenyekiti aliendelea kueleza kuwa nchi kadhaa duniani zimeshindwa kufanya Muungano lakini Tanzania imeweza kuufanya na kuudumisha hadi hivi sasa unatimia miaka 49 na kuwataka WanaCCM kutodanganyika na propakanda za aina yoyote juu ya Muungano.
 
Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo yalioikomboa Zanzibar na ndio maana Serikali za awamu zote zimekuwa zikiyaendeleza Mapinduzi hayo hivyo aliwaeleza wanaCCM kuwa ni wajibu wao kuyalinda na kuyadumisha Mapinduzi hayo.
 
Aidha, Dk. Shein amewataka wanaCCM kuendeleza amani na utulivu na kusisitiza kuwa yeyote atakaevuruga na kuvunja amani hiyo basi atashughulikiwa kwa taratibu zote za sheria ziliopo kwani jambo hilo aliliahidi tokea alipokuwa katika kampeni za uchaguzi zilizopita wkati akitafuta ridhaa za wananchi ili wamchague kuiongoza Zanzibar.
 
Katika ziara yake hiyo ya Chama Dk. Shein aliweka mawe ya msingi katika Matawi mbali mbali ya CCM pamoja na mskani za chama hicho sambamba na kupachika bendera za CCM na kupokea wanachama wapya 54 ambao wawili miongoni mwao ni kutoka chama cha  CUF na 52 kutoka CHADEMA.