RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk. Ally Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Taarifa hiyo inasema tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
“…Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.