RAIS wa Tanzania Dk. Pombe John Magufuli amemteuwa Spika mstaafu, Anne Semamba Makinda kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kushika nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Ali Mchumo aliyemaliza muda wake.
Rais Magufuli amefanya uteuzi huo leo ikiwa ni pamoja na kumteuwa Jaji Shabani Ally Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Kabla ya uteuzi huo unaoanza Mei 30, 2016 Jaji Lila alikuwa Jaji Kiongozi.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemteuwa Profesa Apollinaria Elikana Pereka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Kabla ya uteuzi huo Prof. Elikana alikuwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Morogoro.
Profesa Elikana anachukua nafasi ya Profesa Fredrick Mwanuzi ambaye amemaliza muda wake. Uteuzi huo umeanza Mei 30, 2016 kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari.