RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amefuta safari zote za nje ya nchi kwa sasa na badala yake kuwataka watendaji kuanza safari za kutembelea wananchi vijijini ili kujua zaidi changamoto za wananchi na namna ya kuzitatua.
Dk. Magufuli amechukua hatua hiyo alipokuwa akifanya kikao na Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ukiwa na lengo la kutoa uelekeo wa Serikali anayoitaka.
Alisema safari hizo za nje zimefutwa hadi hapo atakapotolea maamuzi mengine huku akisisitiza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje.
Alisema endapo itatokea jambo la dharura sana kwenda nje ya nchi ni lazima kibali kitolewe na Rais au Katibu Mkuu KiongoziBadala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.
“Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘HAPA KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja,” alisema Rais Magufuli.
Katika Kikao hicho, Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni lazima kila mtendaji Serikalini kuuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele kwa ufanisi zaidi. Rais pia ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze kuyasimamia bila kukosa.
Aidha alifafanua kuanzia Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza kuliwekea mikakati tayari kwa utekelezaji, huku akisisitiza kuwa suala lamikopo ya wanafunzi nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi.