RAIS wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli ameendelea kufanya mabadiliko ndani ya serikali yake huku akiziba mianya ya ufujaji fedha usiokuwa wa lazima kwa kufanya mabadiliko mengine kwa siku kuu ya 9 Desemba kuwa siku ya Uhuru na Kazi.
Rais Dk. Magufuli amefanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria ya Siku kuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka rais kutangaza siku yoyote kuwa siku kuu au mapumziko. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi hasa kufanya usafi wa maeneo mbalimbali.
“…Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.”
Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, hivyo fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali na vinginevyo kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.
“…Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016,” ilieleza taarifa ya Ikulu.