RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Oktoba 3, 2013 amezindua miradi miwili mikubwa ya maendeleo Kisiwani Mafia ambayo inamaliza kero za miaka mingi za wakazi wa Kisiwa hicho.
Rais Kikwete amezindua Uwanja wa Kisasa wa Ndege wa Mafia na pia amefungua Gati ya Mafia, miradi mikubwa ya miundombinu iliyoko mjini Kilindoni na ambayo inamaliza malalamiko ya miaka mingi ya usafiri ya wakazi wa Mafia.
Ndege iliyombeba Rais Kikwete imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mafia kiasi cha saa 5:35 asubuhi na kuanza mara moja shughuli ya kuzindua Uwanja huo ambao umejengwa kwa gharama za dola za Marekani milioni 13.57.
Uwanja wa Ndege wa Mafia ni moja ya miradi mingi na mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa nchini chini ya misaada ya Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) na ambayo katika Tanzania utekelezaji wake uko chini ya Akaunti ya Changamoto za Milenia Tanzania ya Millennium Challenge Corporation Tanzania (MCA(T).
Hiyo ndiyo imekuwa shughuli ya kwanza kufanywa na Rais Kikwete ambaye ameanza ziara ya siku tano ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani kwa kutembelea Kisiwa cha Mafia.
“Bado tunayo kazi ya kufanya kuhusu uwanja huu wa Mafia ikiwa ni pamoja na kuuwekea taa, ili uweze kutumika hata usiku, na pia kujenga jengo jipya la kisasa la abiria ili kuongeza uwezo wa usafiri wa Kisiwa cha Mafia kuliko ilivyo sasa,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:
“Najua kuwa wakazi wa Mafia, kwa miaka mingi mmekuwa na vilio viwili vikubwa vinavyohusiana na miundombinu, usafiri na mawasiliano ya usafiri – yaani uwanja wa ndege na gati. Yote mawili sasa tumeyafanikisha na kuyatekeleza kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2013. Ndugu zangu wa Mafia kimebakia nini sasa?” amesema Rais Kikwete na kuelezea jitihada za Serikali za kujenga viwanja vya ndege nchini.
Kwenye Bandari ya Kilindoni, Rais Kikwete amezindua Gati ya Mafia ambayo ina urefu wa kilomita 1.3, uwezo wa kubeba magari yenye tani zisizozidi 10 na yanayokwenda kwa kasi ya maili 15 kwa saa, mradi ambao umegharimu kiasi cha Sh. bilioni 20.
Baada ya kuzindua rasmi Gati hiyo, Rais ametembea urefu nzima wa daraja hilo ambako aliwapokea abiria wa kwanza kutumia Gati hiyo na kuwasalimia wafanyakazi wa Meli ya F.B. Khadija ambayo itakuwa inatoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati, Mkoa wa Pwani pia.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria shughuli za ujenzi huo, Rais Kikwete amefurahi kuwa Serikali yake imeweza kumaliza kero mbili kubwa na za muda mrefu ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi wa Mafia.
Rais Kikwete ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambayo imejenga na inamiliki Gati hiyo kuweka usafiri wa kuwavusha wasafiri kutoka Gatini hadi meli zinapoegeshwa na kutoa changamoto kwa Mamlaka hiyo sasa kujenga Bandari kamili hapo hapo Mafia. Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam jioni ya leo na kesho ataendelea na ziara ya Mkoa huo wa Pwani kwa kutembelea Wilaya ya Mkuranga.