Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza mshituko wake mkubwa na huzuni yake nyingi, akiomboleza kifo cha Mbunge wa Ludewa, Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Deo Filikunjombe ambaye alifariki katika ajali ya helikopta usiku wa kuamkia Ijumaa, Oktoba 16, 2015 katikati ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous, Mkoa wa Morogoro.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda, Rais Kikwete amesema “Nimeshtushwa mno na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Deo Filikunjombe. Kwa hakika, ni msiba ulionihuzunisha sana.”
Rais Kikwete amemweleza Mama Makinda: “Tumempoteza kijana hodari na mmoja wa wabunge mahiri ambao mchango wao katika Bunge letu tukufu na katika shughuli za uongozi wa nchi yetu na wananchi wake zilikuwa zinajionyesha dhahiri. Ni kifo ambacho kimetuachia pengo kubwa la uongozi na kimetokea wakati bado Bunge lako tukufu, Chama chetu cha CCM na wananchi wa Ludewa walikuwa bado wanahitaji uongozi na mchango wake.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Spika wa Bunge letu tukufu salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao. Aidha, kupitia kwako nawatumia wananchi wa Ludewa salamu zangu nyingi za rambirambi kwa kumpoteza Mbunge wao aliyewatumikia vizuri na kwa moyo wote kwa kipindi chote cha miaka 10 ya Ubunge wake.”
“Aidha, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi kwa familia ya Mheshimiwa Filikunjombe pamoja na ndugu na marafiki wa familia hiyo. Naelewa machungu ya familia kwa kuondokewa na mhimili wao. Wajulishe Wabunge, wajulishe Wana-Ludewa na ijulishe familia ya Marehemu Filikunjombe kuwa niko nao katika maombolezo ya msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu. Napenda pia wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehemu Deo Filikunjombe. Amen.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete Jumamosi asubuhi, Oktoba 17, 2015, aliungana na mamia ya wananchi na waombolezaji kuuaga mwili wa Mheshimiwa Filikunjombe katika shughuli iliyofanyika kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, mjini Dar es Salaam.