Na Mwandishi Maalumu, Ghana
RAIS John Evans Atta Mills wa Ghana ambaye amezikwa,
Agosti 10, 2010, alibashiri kifo chake na kuwaachia wananchi wa Ghana
wosia wa kuwaaga, akiwaasa kukataa vurugu nchini humo, na akiwataka
kulinda na kudumisha amani ya nchi hiyo hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao Desemba mwaka huu.
Katika wosia huo ambao haijulikani aliuandika lini, ingawa inafikiriwa
ni baada ya kuambiwa kuwa maisha yake duniani yalikuwa mafupi kutokana
na ugonjwa wa kansa ya koo, Rais Mills aliwaaga wananchi wenzake wa
Ghana kwa kuwaambia: “Kwaherini kaka na dada zangu”.
Sehemu fupi ya ujumbe huo uliokuwa kwenye vipeperushi ulisambashwa kwa helikopta kwenye uwanja wa Independence Square mjini Accra ambako
kwa maelfu na maelfu ya waombolezaji walishiriki katika ibada na
shughuli maalum ya mazishi ya Rais Mills.
Katika ujumbe huo, Rais Mills ambaye aliaga dunia Julai 24, mwaka huu,
miezi mitano tu kabla ya kuwania kushinda kipindi cha pili cha miaka minne cha uongozi wake alisema: “Nilikuja kutumikia; nimemaliza muda wangu hapa duniani na sasa naingia katika mapumziko ya milele na kuanza utumishi wa majukumu yangu na Baba Yangu wa Mbinguni. Wakati unapitia kurasa hizi za maisha yangu, namwomba Mwenyezi Mungu kwamba historia hii ya maisha yangu ikuguse kwa njia nyingi njema.”
Ameongeza Rais Mills katika wosia wake “Mimi mzima na niko macho mbele ya Muumba wangu. Kamwe Ghana haitakufa. Ghana itabakia hadi itakapotangaza ufalme wa Muumba”. “Wakati napumzika katika amani iliyokamilika mikononi mwa Muumba wangu, nawaahidi kuwa milele nitaendelea kutangaza na kulinda jina zuri la Ghana. Mkumbuke Muumba katika njia zako zote, na Atakulinda. Kaeni kwa amani kaka zangu na dada zangu, kwa sababu daima nitakuwa na nyie”. Aliandika Rais Mills kabla ya kufariki dunia.
Wosia huo umetiwa saini kwa jina la John Evans Atta Mills na
ulisambazwa kwenye moja ya nyaraka zake nyingi zilizosambazwa kwa
waombolezaji leo katika kitabu kilichoitwa “kumbukumbu”.
Katika wosia mfupi zaidi ambao ulisambazwa kwa njia ya vipeperushi kwa wananchi walioshiriki shughuli za mazishi yake, Rais Mills aliwaambia wananchi wa Ghana: “Ishi katika Ndoto. Pigania Amani. Kataa Vurugu Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2012. Kwaherini kaka zangu na dada zangu.”
Ghana inafanya Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba mwaka huu na Rais Mills tayari alikuwa ameteuliwa na chama chake cha NDC kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa mara ya nne mfulilizo.
John Evans Fiifi Atta Mills aliapishwa kwa mara ya kwanza
kuwa Rais wa Ghana Januari 7, 2009, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa
Desemba 2008 ambako alikuwa anawania nafas hiyo kwa mara ya tatu
mfululizo.