Rais Andry Rajoelina Awasili Tanzania kwa Mazungunzo na JK

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akimlaki Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar Mhe Andry Rajoelina aliyewasili Mei 3, 2013 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina wakati wa mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam Mei 3, 2013. PICHA NA IKULU

RAIS wa Serikali ya Mpito ya Madagascar Andry Rajoelina amewasili mjini Dar es Salaam jioni ya Mei 3, 2013 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete usiku Mei 3, 2013, amefanya mazungumzo na Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar Rajoelina kuhusu hali ya kisiasa ilivyo nchini Madagascar.
Katika mazungumzo hayo yaliyokwenda vizuri na kufanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Rajoelina amemweleza Rais Kikwete kuhusu hali ya kisiasa ilivyo katika nchi hiyo ambayo inajiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu Julai 24, mwaka huu.
Mahakama Maalum ya Kikatiba ya Madagascar mchana wa leo imepitisha majina ya wagombea 41 wa nafasi ya Urais wa nchi hiyo, akiwemo Rais Rajoelina, kati ya wagombea 50 waliokuwa wameomba kuwania nafasi hiyo.
Rais Rajoelina amewasili nchini jioni ya jana kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ambaye amepewa jukumu la usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kuendelea na mazungumzo yao leo, Jumamosi, Mei 4, 2013, asubuhi kabla ya Rais Rajoelina hajaondoka nchini kurejea nyumbani. Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi yaa Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Anakutana na Rais Rajoelina kwa mara ya tatu sasa, mara ya kwanza ikiwa ni mwezi Desemba mwaka jana, na baadaye mwezi Januari mwaka huu.

Rais Kikwete alipokutana mara ya mwisho na Rais huyo wa serikali ya mpito ya Madagascar alifanikiwa kumshawishi akubaliane na mapendekezo ya nchi za SADC kuwa asigombee kwenye uchaguzi mkuu utaofanyika mwaka huu kama njia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo. Rais Kikwete awali ya hapo aliweza pia kumshawishi Rais wa zamani wa Madagascar Mhe Marc Ravalomanana asigombee katika uchaguzi mkuu huo.