Na Mtuwa Salira, EANA Arusha
MATOKEI ya kwanza ya utafiti juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeonyesha kwamba jumuiya hiyo iliundwa kama chombo kilichoandaliwa kuwepo kwa maslahi ya serikali na wafanyabiashara wakubwa.
Jumuiya hiyo yenye wananchama watano ingawa ilianzishwa upya kuwa ‘’jumuiya yenye misingi ya watu’’ wenyewe wa Afrika Mashariki, imebainika ushiriki wa raia wa kawaida katika mchakato wa mtagamano huo ni mdogo mno. Wanachama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wataalam la Afrika Mashariki (VEAF), lililofanya utafiti huo imebaini pamoja na mambo mengine kwamba mpaka sasa mwenendo wa ushirikiano huo ni kutoka juu kwa watawala kwenda chini huku raia wengi wakawaida wakiwa hawana taarifa juu yake, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki linaripoti.
“Theluthi moja ya watu kama wa Tanzania na Kenya hawajahi kusikia juu ya mtangamano wa EAC,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya VEAF, Dr Azaveli Lwaitama.
“Ni kwa kuboresha uelewa wa raia juu ya mwenendno mzima wa ushirikiano kwa kushughulikia hofu za wananchi wa pande zote za nchi husika, ndipo awamu hii ya pili ya kihistoria ya kurejesha upya jumuiya hiyo inaweza kufanikiwa,” taarifa ilisisitiza.
EAC ilizinduliwa upya mwaka 1999 baada ya jumuiya ya kwanza kuvunjika mwaka 1977 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo tofauti za kisiasa na kiuchumi miongoni mwa wanachama watatu wa awali wa jumuiya hiyo, Kenya, Uganda na Tanzania.
Ripoti kamili ya utafiti huo kwa mujibu wa taarifa hiyo itazinduliwa rasmi leo na Rais wa zamani wa Tanzania Alli Hassan Mwingi katika hoteli ya Holiday Inn, jijini Dar es Salaam ambapo pia Katibu Mkuu wa zamani wa EAC, Balozi Juma Mwapachu atakuwa mmoja wa washiriki muhimu katika uzinduzi huo. Sherehe za uzinduzi na matokeo ya kwanza ya utafiti huo umefadhiliwa na Taasisi ya moja ya Ujerumani ya Frieddrich-Ebert-Stifstung (FES) tawi la Tanzania.