Na Mwandishi Wetu,
MWENYEKITI wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Aden Rage ameligomea Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura ndani ya siku 14. Rage ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na waandishi wa Habari kuzungumzia agizo hilo la TFF pamoja na lile la Kamati ya Utendaji ya Simba iliyomsimamisha uenyekiti siku chache zilizopita.
“Kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokaa na kuamua kunisimamisha ni batili kwa kuwa aliyeitisha mkutano huo hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa Katiba ya Simba, hivyo ni sawa na kikao cha harusi,” alisema.
Alisema anaishangaa TFF kumpa siku 14 aitishe mkutano wa dharura wakati taasisi hiyo ilipaswa kupinga kitendo cha yeye kusimamishwa nafasi yake ya uenyekiti maamuzi yaliyofanyika kinyume na taratibu za michezo yaani kufanya mapinduzi.
Alisema kutokana na kukiukwa kwa Katiba ya TFF na klabu ya Simba, hatoitisha mkutano wowote kama alivyotakiwa ili naye asivunje Katiba na kama atalazimishwa kufanya hivyo yuko tayari kujiuzuru nafasi yake kuliko kusimamia kuvunja katiba.
Rage alitolea mfano wa msuguano uliotokea katika kipindi cha uchaguzi wa TFF ulioifanya Serikali kuingilia kati sanjari na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa), alisema baada adha hiyo kutokea Fifa iliamuru TFF iitishe uchaguzi na kuwapangia tarehe na agenda.
Aliongeza kuwa kutokana na TFF kumuagiza kuitisha mkutano ndani ya Siku 14 pamoja na kumchagulia agenda ni kinyume cha Katiba ya TFF, hivyo hatoitisha mkutano kama alivyotakiwa na shirikisho hilo.
Hata hivyo Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura alipotakiwa kufafanua ni hatua gani zitachukuliwa ikiwa Rage atagoma kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura kama alivyoagizwa, alisema wao bado wanasubiri siku 14 zikamilike ili kuchukua hatua nyingine za kuchukua endapo Rage hatotekeleza maagizo yao.
“Tunashukuru kuwa amekiri kupokea barua yetu, hivyo tunasubiri hadi siku 14 ziishe ndio itajulikana TFF nini itafanya dhidi yake, tusubiri muda uishe na leo ni siku ya pili,” alisema Wambura.
TFF juzi ilitoa agizo la kumtataka Rage aitishe Mkutano Mkuu wa dharura kwa kutumia Ibara 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema, “Simba Sports Klub ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na Fifa na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”
Rage katika mkutano huo, alimtangaza pia Richard Wambura kuwa ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu ya Simba. Akizungumzia suala la kusaini Mkataba na Azam TV alisema suala hilo halihitaji shule kwa kuwa mhusika Mkuu ni TFF, hivyo iwe isiwe ni lazima klabu isaini na ndio sababu alifanya hivyo miezi minne iliyopita na klabu kupewa mil 100.