Promota ‘Kaike Siraju’ Adaiwa Kuwaingiza Mitini Mabondia

Promota Kaike Siraju (kulia) akishuhudia mabondia Fadhiri Majia na Nassib Ramadhan, wakitiliana saini kataba wa kucheza pambano lao lililofanyika June 9, 2012. Promota huyo ndiye anayedaiwa kuwaingiza mitini mabondia wanne.

Na Mwandishi Wetu

PROMOTA wa ngumi za kulipwa nchini Kaike Mfaume Siraju anadaiwa kuwaingiza mitini mabodia wanne vijana nchini Tanzania baada ya kuwapambanisha Julai 15, 2012 kwa makubaliano ya kuwalipa malipo kidogo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata inadaiwa promota Siraju mnamo Juni 25, 2012 aliwasainisha mkataba mabondia wanne (Issa Omar kucheza na Ramadhan Kumbele na Mwaite Juma kucheza na Anthony Mathias) mbele ya Katibu Mkuu wa Ngumi za Kulipwa Tanzania, Ibrahim Kamwe kwa makubaliano ya kuwalipa sh. 80,000 jambo ambalo hakulifanya.

Taarifa zinasema Siraju amekewa akiwazungusha mabondia hao kila wakati hadi walipokata tamaa na kuamua kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Ngumi za Kulipwa Tanzania, Kamwe na alipojaribu kufanya mazungumzo naye hali ya kuwazungusha iliendelea kama ilivyo kuwa awali.

Kamwe amethibitisha mabondia hao kuingizwa mitini na promota huyo huku akidai amejaribu kwa juhudi zake kufuatilia na hata kukutana na promota huyo bila mafanikio. “…Ni kweli vijana hao walicheza na hawakulipwa, kwani baada ya pambano alitoroka (promota), walipojaribu kumdai haki yao kwa siku zilizofuatia walipigwa kalenda na kuwatembezatembeza kwa usumbufu…mara kuwaambia wamtafute mara Mango Garden…,” alisema Kamwe katika maelezo yake.

Aidha alisema baada ya vijana kuzungushwa bila mafanikio walimjulisha Katibu Mkuu naye kujaribu kuwasiliana promota huyo bila mafanikio. “Mambo yanayofanywa na Kaike si ya kiungwana ni kuwavunja moyo mabondia chipukizi, kudumaza ngumi na kufanya mchezo wa ngumi uonekane ni mchezo wa wahuni…,” alisema Katibu Mkuu.

Hata hivyo juhudi za kumpata promota huyo zinafanywa ili kueleza sababu ya kuwaingiza mitini vijana hao.