Profesa Mwandosya atoboa siri ya afya yake

Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya akizungumza na wanahabari jana.

Na Magreth Kinabo, Maelezo na Bujo Ambosisye (MoW)

WAZIRI wa Maji, Profesa Mark Mwandosya ambaye alikuwa amelazwa Hospitali ya Apollo, nchini India, amesema hajawahi kuugua na kulazwa hospitalini kwa miaka 34 akiwa mtumishi wa umma.

Profesa Mwandosya, aliyasema hayo Desemba 03, 2011 akizungumza kwenye mkutano na watendaji wakuu, baadhi ya watumishi wa Wizara yake na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza baada ya kurejea nchini akitokea India kwenye matibabu.

Katika mkutano huo, Prof. Mwandosya alianza kwa kumshukuru Mungu kwa rehema zake kwani kwa sasa hali yake inaendelea vizuri. Aliongeza kuwa fimbo aliyonayo ataitumia kwa muda mfupi wakati viungo vyake vinatengemaa.

“Baada ya kutangaziwa tanzia nakiri kuwa anayezungumza ni mimi mwenyewe wala siyo mzimu wangu, nimerudi nyumbani salama baada ya kutibiwa kwa miezi mitano na nusu,” alisema, Prof. Mwandosya.

Aidha Prof. Mwandosya alimshukuru Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sherif Hammad, Spika wa Bunge Anna Makinda, mawaziri wote, wabunge wote na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahimu Lipumba, kwa kumjulia hali kwa njia ya simu pamoja na mtandao na wengine kumtembelea moja kwa moja.

“Nimeona niitumie fursa hii kuwashukuru nyie wadau wa sekta ya maji kwa kuendelea kufanya kazi wakati mimi nilikuwa sipo. Sekta ya maji inaendelea vizuri,” alisisitiza.

Profesa Mwandosya aliongeza kuwa kitu kilimchompa nguvu ni upendo na ubinadamu alionyeshwa na Watanzania.

“Hili nakiri sikulitegemea nilidhani ningepata lawama kwa kutotimiza adhima ya huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi, lakini ajabu nilioneshwa upendo, ubinadamu na mshikamano na wananchi wa kawaida kutoka mikoa mbalimbali kwa njia ya simu na mtandao. Hii ilinipa faraja,” alisema huku akisisitiza tusipoteze upendo, ubinadamu na mshikamano huo.

Aliwashukuru waandishi wa habari kwa kuwajulisha wananchi jinsi alivyokuwa anaendelea akiwa nchini India, Viongozi wa dini kwa sala maalum za kumwombea na wananchi wote kwa kumjulia hali na kumwombea. Aidha, alitoa shukrani zake za pekee kwa wapiga kura wake wa jimbo la Rungwe Mashariki na kuwapongeza kwa kupata Halmashauri mpya ya Busokelo.

Prof. Mwandosya aliruhusiwa na daktari wake kutoka hospitalini Apollo Novemba 28, ambapo aliondoka India Novemba 29, kabla ya kuwasili nchini Desemba Mosi, mwaka huu kwa ndege ya Shirika la la Emirates.